• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
Mbunge sasa ataka Wameru wawe na chama chao cha kisiasa

Mbunge sasa ataka Wameru wawe na chama chao cha kisiasa

NA MWANDISHI WETU

BAADHI ya viongozi katika kaunti ya Meru wamezindua tena miito ya kuundwa kwa chama chao cha kisiasa kitakacho jali maslahi wakazi wa eneo la Mlima Kenya Mashariki wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022.

Kampeini za “chama chetu wenyewe” zinaongozwa na Mbunge wa Imenti kusini  Bw Kathuri Murungi anasema ipo haja kwa viongozi wa eneo hilo kuunda chama kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2022..

Matamshi hayo yameungwa mkono na Mbunge wa Imenti kaskazini Bw Rahim Dawood  aliyesema sharti chama kiundwe  kuzingatia maslahi ya wakazi wa eneo la Mlima Kenua mashariki.

Bw Murungi amesema kuwa eneo hilo litakosa nyadhifa za juu serikalini ikiwa haina chama chake kitakacho dhamini wawaniaji viti.

Pia alisema itakuwa rahisi kwa eneo hilo kusukuma kuzinduliwa kwa miradi ya maendeleo wakiwa na chama chao.

“Lazima tuungane pamoja ndipo tufikiriwe wakati wa ugavi wa nyadhifa serikalini.Siku za usoni lazima tujitetee tupewe nyadhifa za juu ikiwa ni pamoja na kuteuliwa kwa mmoja kutoka eneo hili kuwa Spika katika Bunge la Kitaifa na Bunge la Seneti,” alisema Bw Murungi.

Mbunge huyo aliyewania kiti kwa tikiti ya kibinafsi baada ya kung’atuka na kukihama chama cha Jubilee alisema mwaka huu miungano mingi ya kisiasa itabuniwa kushirikiana na vyama tanzu vya kisiasa.

“Ninaamini 2019 utakuwa mwaka wa kuundwa kwa miungano mikuu. Maeneo yaliyo na vyama tanzu vya kisiasa itafaidi pakubwa. Wakati umewadia na ni sasa tufikirie hatma ya eneo hili kisiasa,” Bw Murungi.

Alisema kaunti ya Meru iko na idadi kubwa ya wapiga kura na itajishinikiza kisiasa ikiwa itakuwa na chama chake cha kisiasa.

“Nawahimiza viongozi kutoka eneo hili wazingatie wazo hili la kuundwa kwa chama cha kisiasa kwa lengo la kujiimarisha kisiasa,” alisema mbunge huyo.

Bw Murungi alisema ijapokuwa chama cha PNU kiko na uungwaji mkono mkuu kaunti ya Meru, bado kinakumbwa na mizozo ya ndani inayokiyumbisha.

Kumekuwa na juhudi za kurejesha uongozi wa chama hicho kwa rais mstaafu Mwai Kibaki kutoka kwa kundi linaloongozwa na Waziri wa Biashara Peter Munya.

Lakini katibu mkuu wa PNU John Okemwa amesema chama hicho kiko imara licha ya majaribio kurudisha uongozi kwa Bw Kibaki.

“Nawakikishia wafuasi wetu Meru kuwa kwamba uongozi wa PNU haujabadilishwa. Kile kiko ni mvurugano unaoongozwa na wale wanaojaribu kutwaa uongozi,” Bw Okemwa alisema.

Alisema mabadiliko makubwa yatafanyiwa chama cha PNU mwaka huu mpya hasa baada ya kutwaa tena makao yake makuu kutoka kwa chama cha Jubilee.

“PNU kingali mikononi mwa viongozi waliotwaa uongozi kutoka kwa Bw Munya. Sasa tunajaribu kumsaidia Rais kufanikisha ajenda zake kuu nne,” alisema Bw Okemwa.

You can share this post!

Equity kufadhili masomo ya wanafunzi 12 wa Trans Nzoia

NYS sasa kutegemea mapato yake kujiimarisha

adminleo