• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
Ongwae akanusha njama ya kuilaghai Serikali Sh54 milioni

Ongwae akanusha njama ya kuilaghai Serikali Sh54 milioni

Aliyekuwa meneja mkurugenzi wa Kebs Charles Ongwae. Picha/ Richard Munguti

Na Richard Munguti

ALIYEKUWA mkurugenzi mkuu wa shirika la ukadiriaji ubora wa bidhaa nchini (Kebs), Bw Charles Ongwae alishtakiwa Jumatano kwa kujaribu kuilaghai serikali zaidi ya Sh54 milioni.

Bw Ongwae alifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot na kukanusha mashtaka dhidi yake ya kufanya njama ya kuilaghai Serikali mamilioni ya pesa kupitia uingizaji wa bidhaa za mafuta nchini kinyume cha sheria.

Bw Ongwae aliamriwa ajisalamishe kwa afisa anayechunguza kesi hiyo katika afisi ya Mkurugenzi wa Jinai (DCI) mnamo Januari 7, 2019 kuandikisha taarifa.

“Bw Ongwae hajaandikisha taarifa katika afisi ya DCI,” alisema kiongozi wa mashtaka, Bi Annette Wangia.

Akaongeza : “Mshtakiwa alijisalamisha mahakamani kabla ya alama zake za vidole kuchukuliwa na kuandikisha taarifa kuhusu kesi hii. Naomba afike katika afisi ya DCI Ijumaa .”

Kiongozi wa mashtaka Bi Annette Wangia akisoma faili. Picha/ Richard Munguti

Bw Ongwae alipinga ombi la kumtaka ajisalamishe Ijumaa (kesho) akisema tabia ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma kuwazuia wakuu wa mashirika ya serikali na maafisa wa serikali katika kampeni yake ya “ kamata kamata” haipasi kuruhusiwa kuendelea.

“Naomba hii mahakama inikubalie kujisalamisha kwa DCI Januari 7, 2019 kwa vile mpango wa DPP wa “Kamata Kamata” wa Ijumaa unahujumu haki za washukiwa,” alisema Bw Ongwae.

Lakini hakimu alishangaa sababu ya DPP kuwazuilia siku za Ijumaa na akakubaliana na mshtakiwa kwamba “ Januari 7, 2019” inafaa.

Mshtakiwa aliagizwa afike mbele ya afisa anayechunguza kesi hiyo mnamo Januari 7, kuandikisha taarifa.

Mahakama ilimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh500,000 na kumwamuru afike kortini Januari 23, 2019 kesi hiyo itakapotajwa.

Mahakama ilielezwa kuwa, kesi dhidi ya Bw Ongwae itaunganishwa na nyingine ambapo washukiwa wengine 13 walishtakiwa Jumatatu wiki hii.

“Kesi hii itaunganishwa na nyingine ambapo washukiwa wengine walishtakiwa Jumatatu. Watafika mahakamani Januari 23, watengewe siku ya kusikizwa kwa kesi,” alisema Bi Wangia.

Washtakiwa hao 14 wamekanusha mashtaka ya kuingiza bidhaa za mafuta humu nchini bila kulipia ushuru.

Washtakiwa hao walifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku.

Bw Ongwae hakufika siku hiyo na mawakili wake wakaomba kibali cha kumtia nguvuni kisitolewe dhidi yake kwa vile alikuwa amehudhuria mazishi.

Hata hivyo, mahakama iliamuru washukiwa wawili Mabw Hillary Kamau na Alex Maina Nderitu watiwe nguvuni.

Bw Mburu pamoja na Bw Kamau ambao ni wakurugenzi wa kampuni ya Landmark Freight Services Limited walishtakiwa kwa kuficha mafuta waliyioingiza humu nchini kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru.

You can share this post!

Aliyeingiza mabinti Wapakistani nchini kiharamu akamatwa

Wasichana wa Narok kuchunguzwa kama wamekeketwa

adminleo