Mutuma Mathiu ateuliwa Mkurugenzi Mhariri mpya NMG
NA FAUSTINE NGILA
KAMPUNI ya Nation Media Group Plc (NMG) Alhamisi ilimteua aliyekuwa mhariri msimamizi wa gazeti la Daily Nation Bw Mutuma Mathiu kuwa Mkurugenzi Mhariri wa vyombo vyote vya habari vya kampuni hiyo Afrika Mashariki.
Kwenye taarifa rasmi ya uteuzi huo, kampuni hiyo ilisema Bw Mathiu atasimamia shughuli zote kuhusu maadili ya uanahabari, sera za uhariri, sera za usambazaji wa matini kwenye masoko mbalimbali na sera ya kuboresha vipaji vya wanahabari.
“Bw Mathiu atatwaa cheo hiki kuanzia Januari 1, 2019 na kuacha cheo cha awali cha mhariri mkuu wa gazeti la Daily Nation. Alijiunga na kampuni hii mwaka 1997 kama mhariri msanifishaji wa Sunday Nation na kupandishwa cheo kuwa Meneja Mhariri wa Sunday Nation na kisha Daily Nation,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa NMG Bw Stephen Gitagama kwenye uteuzi wake.
Kwa wakati mmoja Bw Mathiu alikuwa Meneja Mhariri katika kampuni ya Mwananchi Communications Limited nchini Tanzania inayomilikiwa na NMG, na inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen.
Bw Mathiu alichukua nafasi hiyo baada ya aliyekuwa Mhariri Mkuu Bw Tom Mshindi kustaafu mnamo Desemba 31, 2018.
Mwanahabari huyo mpevu amesomea Shahada ya Sanaa katika Chuo Kikuu cha Egerton, Stashahada ya Uanahabari katika Chuo Kikuu cha Nairobi na shahada ya Uzamili ya Sanaa katika Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza.
NMG inamiliki vyombo vya habari katika mataifa yote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki isipokuwa Burundi. Hii ndiyo kapuni kubwa zaidi ya uanahabri katika kanda hii.
Humu Kenya NMG inamiliki magazeti ya Taifa Leo, Daily Nation, Business Daily, The East African na Mwanaspoti. Runinga yenye wafuasi wengi zaidi mitandaoni ya NTV pia ni mali yake.