Viongozi wakataa utaratibu wa kugawa fedha za kaunti

Na BRIAN OKINDA

VIONGOZI kutoka kaunti za kaskazini mwa nchi wamepinga vikali mbinu mpya ya kugawa fedha kwa kaunti inayopendekezwa na Tume ya Ugavi wa Fedha kwa Kaunti(CRA).

Wamesema kwamba utaratibu huo utakaotumika kugawa Sh335.6 bilioni kwa kaunti zote 47 ni ya kibaguzi na imefeli vigezo vya usawa.

Viongozi hao walitoa wito kwa wenzao katika kaunti nyingine kukataa fomyula hiyo na kuahidi kwamba wataelekea mahakamani kuipinga iwapo itapitishwa na kutekelezwa jinsi ilivyo.

Aidha, walidai kuwa uongozi wa kaunti za maeneo kame ukiungwa mkono na Baraza la Maendeleo la kaunti hizo (FCDC) na Kundi la Wabunge kutoka Jamii ya Wafugaji (PPG) watafuatilia suala hilo kwa kutumia njia za kisiasa ili kuliangusha katika mabunge ya seneti na ya kitaifa.

“Tume ya CRA haijatoa wala kueleza vigezo vilivyotumika kufikia fomyula hiyo mpya na badala yake waliegemea sana idadi ya watu wakifikiria kwamba maeneo yote nchini yana kiwango sawa cha maendeleo,” akasema Mwenyekiti wa FCDC Ali Roba ambaye pia ni Gavana wa Mandera.

Bw Roba alidai kuwa kaunti hizo zitapoteza zaidi ya Sh100 bilioni iwapo fomyula hiyo mpya itatumika na kutaka tume hiyo kusubiri hadi sensa ya mwaka ujao ifanyike ndipo iamue jinsi fedha hizo zitakavyogawanywa.

Habari zinazohusiana na hii

Maskini kupigwa kiboko

Bei ya unga kushuka

FEDHA: Wizara ya nuksi