Habari MsetoSiasa

Waititu amtuma nduguye Moses Kuria likizo ya lazima zogo likitokota

January 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na Erick Wainaina

SIKU moja tu baada ya Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria kusema kwamba eneo la Mlima Kenya halijafaidika sana na serikali ya Jubilee ikiwa mamlakani, Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu amemtuma kwa likizo ya lazima nduguye mbunge huyo.

Hatua hiyo inaonekana kama mtindo uliozoeleka unaotumiwa na gavana huyo kuwaadhibu maadui wake kisiasa.

John Ngigi Kuria, ambaye ni afisa mkuu wa kilimo katika serikali ya kaunti alitumwa kwa likizo ya lazima ya siku 30 kupitia barua iliyotiwa saini na Bw Waititu huku akiamrishwa kusalimisha vifaa vyote vya kazi na mali ya kaunti iliyokuwa chini ya usimamizi wake.

Bw Kuria wakati wa sherehe za kukaribisha mwaka mpya katika uwanja wa kaunti ndogo ya Thika alilalamika kwamba ingawa eneo hilo liliunga mkono Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto katika chaguzi za mwaka wa 2013 na 2018, hakuna maendeleo ya maana yaliyoafikiwa. Bw Waititu pia alihudhuria hafla hiyo.

Hata hivyo nduguye Januari 2 alipata barua iliyomwaamrisha kuenda likizo ya lazima.

“Unashauriwa uende likizo ya lazima ya kila mwaka kwa siku 30 kuanzia Alhamisi Januari 3, 2019. Kwa mantiki hii unaombwa kumkabidhi majukumu yako na vifaa vya kazi kwa afisa mkuu wa mifugo, uvuvi na huduma za matibabu ya wanyama,’ ikasema sehemu ya barua hiyo.