Habari Mseto

Mwanasiasa mchanga kutoka Lamu anayetamba kwa uongozi Barani Afrika


AHMED Omar Hamid, almaarufu ‘Medo’ ni miongoni mwa wanasiasa wachanga zaidi katika Bunge la Kaunti ya Lamu ambaye umaarufu wake unazidi kuenea kila kukicha, si Lamu tu bali pia Pwani, Kenya na Bara zima la Afrika.

Akiwa na umri wa miaka 29, Bw Medo alianza siasa zake 2016 kwa wakati huo akiwa na miaka 22 pekee.

Ni mwaka huo ambapo alitwikwa jukumu la kuwa Mshirikishi wa Vijana kwenye kampeni ya kiti cha ugavana wa Lamu naye mgombea kiti hicho ambaye pia ndiye gavana wa sasa, Bw Issa Abdalla Timamy wa chama cha Amani National Congress (ANC).

Ujasiri wake katika kampeni hizo pia ulimfanya Bw Medo kuongoza kampeni za juu zaidi, hasa zile za kiti ch urais kupitia ANC katika harakati za kumsaidia kiongozi wa chama hicho, Bw Musalia Mudavadi.

Ahmed Omar Hamid, almaarufu Medo (kushoto) akiwa na diwani wa wadi ya Mkomani, Shekhuna Abbas. Bw Medo ni mwanasiasa mchanga wa Lamu anayetamba kwa kushikilia vyeo kitaifa na kimataifa. PICHA|KALUME KAZUNGU

Kwa sasa Bw Mudavadi ndiye Mkuu wa Mawaziri nchini ilhali uongozi wa chama cha ANC kitaifa ukiachiwa gavana wa Lamu, Issa Abdalla Timamy.

Aidha Bw Medo anavuma sana ndani na nje ya Kaunti ya Lamu kutokana na ukuruba alio nao na Gavana Timamy.

Bw Medo anahudumu kama diwani maalum wa chama cha ANC katika Bunge la Kaunti ya Lamu.

Weledi wake wa kujadili, kuchanganua na kutetea masuala mbalimbali, ikiwemo miswada ya maendeleo na kupigania jamii yake ya Lamu bungeni umemfanya kuibuka kupendwa na wengi eneo hilo.

Licha ya umri wake mdogo, Bw Medo tayari ametwikwa majukumu na vyeo kadhaa vizitovizito katika ngazi za kitaifa na kimataifa.

Kwanza, yeye ni mwanachama wa Muungano wa Vijana na Demokrasia Afrika-yaani Young Democrat Union of Africa (YDUA).

Muungano wa Vijana na Demokrasia Afrika

YDUA ni muungano unaojumuisha au kuwaleta pamoja viongozi wote wa vijana ndani ya Bara zima la Afrika, vikao vyake sanasana vikiandaliwa au kufanyika kwenye jiji kuu nchini Ethiopia, Addis Ababa.

Masuala yanayoangaziwa sana hapa ni vijana na maendeleo, hasa yale yanayofungamana na siasa, vijana kuhusishwa kikamilifu katika mambo ya amani na usalama kwa jumla.

Bw Medo pia ndiye Katibu Mkuu wa kitaifa wa muungano wa madiwani wachanga katika mabunge ya kaunti zote 47 nchini Kenya-yaani Kenya Young Members of County Assemblies (KYMCA).

Pia anashikilia wadhifa wa Mshirikishi wa Vijana katika chama cha ANC Ukanda wa Pwani.

Katika mahojiano na Taifa Dijitali, Bw Medo alisema alijitosa siasani karibu miaka tisa iliyopita, wakati huo akiwa mwanaharakati wa kutetea haki za kijamii.

“Nilianza siasa zangu kupitia uanaharakati wa kijamii. Hata urafiki wangu wa karibu na Gavana Issa Abdalla Timamy ulianza wakati huo punde tulipokutana. Mimi ni mmoja wa waanzilishi wa vuguvugu la Fast Action Movement lililokuwa likipigania raslimali za Wapwani. Hapo ndipo niliamua kupigania cheo cha Mshirikishi wa Vijana wa chama cha ANC na nikafaulu,” akasema Bw Medo.

Anafafanua kuwa ufanisi wake katika siasa na uongozi licha ya umri wake mdogo unatokana na kujitolea kwake katika jukumu lolote lile analokabidhiwa kulitekeleza wakati wowote.

Hata hivyo, Bw Medo anashauri waja, ikiwemo vijana wenzake, kuzingatia na kuuthamini sana uongozi kuliko siasa, akitaja uzalendo, uaminifu na kujitolea kuwa resipe muhimu ya kujipata mbele zaidi kisiasa.

“Mahali nimefikia ni kumshuruku Allah (Mungu) tu ambaye amenipa uwezo wa kutia bidii maishani na kuzingatia uaminifu. Isitoshe, kila mara tunapaswa kulenga sana kuwa viongozi kuliko kuwa wanasiasa. Tukifanya hivyo tutafika mbali. Tuuthamini uzalendo na kujitolea ili tujipate mbele zaidi kisiasa,” akasema Bw Medo.

Anashikilia vyeo kadhaa

Alisisitiza kuwa leo hii yeye anashikilia vyeo kadhaa kitaifa na kimataifa, akisema kuwa ni kile kidogo unachokabidhiwa ambacho ukikitumia vyema kitakuwezesha kukipata au kukifikia kilicho kikubwa hadi kufikia upeo kabisa.

Mbali na siasa na uongozi, Bw Medo pia ni mjasiriamali na meneja wa masuala ya kifedha.

Anataja changamoto kadhaa za kibinafsi anazokabiliana nazo, ikiwemo uhaba wa raslimali za kuudhibiti uongozi, maarifa ya kupima na kuweka sawa baina ya majukumu ya kikazi, yale ya kifamilia, siasa na biashara.

Alipoulizwa kuhusu ndoto yake ya maisha, Bw Medo alisema azma yake kuu ni kwamba siku moja atahudumia au kutumikia wadhifa wa juu zaidi katika taifa la Kenya.

Bw Medo alizaliwa Lamu tarehe 28 Septemba mwaka 1994.

Alijiunga na Shule ya Msingi ya St Kevin Hill Academy na kisha sekondari ya Sheikh Khalifa Bin Zayed mjini Mombasa.

Baadaye aliendeleza elimu yake katika Chuo Kikuu cha Moi, akisomea Digrii ya Biashara, hasa udhibiti wa Masuala ya Baharini (Bachelors in Business Management-Maritime Option).

Kwa sasa, anasomea Uzamifu katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya.

Ana mke na ni baba wa watoto watatu.