MAONI: Ruto achukue tahadhari, hali si hali raia wamechoshwa na ushuru
UMEFIKA wakati Rais Ruto na viongozi wengine wakuu latika serikali ya Kenya Kwanza kujiuliza ikiwa walichaguliwa na mahasla kuwasaidia kuimarisha maisha na kustawisha maendeleo nchini au kufanya maisha yao kuwa magumu kiasi cha kulemewa na gharama ya maisha.
Mikakati ya Ruto kuinua uchumi akitumia sera kandamizi zinazowaumiza raia kwa kuwatoza ushuru wa juu kila mara hata kwa bidhaa muhimu kama vile mkate, mafuta ya kupikia na kadhalika ni mbinu isiyompendelea hata chembe raia maskini.
Sipingi raia kulipa ushuru ila serikali hii inafaa kukomesha matozo ya ushuru wa juu ili kupata fedha za kufadhili miradi ya maendeleo,kulipa madeni na kugharamia matumizi mengine serikalini, wanafaa wasuke mbinu mpya kuwezesha serikali kupata fedha za kuendesha shughuli muhimu na kuboresha maisha ya umma.
Je, kwa nini mahasla wabebeshwe mzigo wa ushuru wa juu ilhali baadhi ya maafisa wakuu wametajwa katika kashfa za ufisadi na ufujaji wa fedha za umma bila kuchukuliwa hatua zifaazo?
Je,tangu serikali hii ishike mamlaka, lipi la kusifiwa wamefanya kusaidia raia maskini?
Kwa maoni yangu,mikakati ya rais kuongeza ushuru kupitia Mswada wa Fedha wa 2024/2025 utamwathiri yeye kisiasa na kuonekana kiongozi mrongo asiyefuatilia kwa makini utekelezaji na utimizaji wa ahadi zake alivyoahidi katika kampeni 2022.
Je,huyu Rais Ruto ni yule yule akiwa naibu rais alikuwa akitangatanga akikosoa rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwa kushindwa kuelewa changamoto zinazowaathiri mahasla?
Lazima ikumbukwe kwamba ni serikali hii tu ambayo imekosa kuelewa ushuru wa juu unathiri pakubwa taifa kiuchumi na kuikosesha wawekezaji wa kigeni wakiepuka mzigo wa ushuru.