Mahangaiko ya wakulima wa pamba ya kisasa licha ya rundo la ahadi
MIAKA sita baada ya Kenya kuidhinisha ukuzaji wa pamba iliyoboreshwa (biotech cotton), kilimo chake kinazingirwa na changamoto anuwai.
Wakulima wengi wangali wanategemea msimu wa mvua kuzalisha bidhaa hiyo muhimu.
Uzalishaji pamba ya kisasa uliidhinishwa 2018 baada ya Mamlaka ya Kitaifa Kuhusu Usalama wa Bidhaa – National Biosafety Authority (NBA), chini ya Kifungu cha 2 cha Sheria ya 2009 kuhusu usalama wa Kibayolojia, kuridhishwa na utafiti uliofanyika.
Aidha, utafiti wa bt cotton ulitekelezwa na Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (Kalro), kwa ushirikiano na asasi husika zingine.
Changamoto kuu inayotishia sekta hii ni wakulima kucheleweshewa mbegu.
Joseph Thika ni mkulima wa zao hili katika Kaunti ya Kirinyaga, na anakiri hukawia kupata mbegu za pamba.
“Shida kubwa inayotuzingira ni uhaba wa mbegu, hatuzipati kwa wakati ufaao,” Joseph akaambia Akilimali Dijitali wakati wa mahojiano shambani mwake Kirinyaga kufuatia hafla iliyoandaliwa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Bioanuwai 2024.
Ikiwa iliandaliwa na Open Forum on Agricultural Biotechnology (OFAB Kenya) kwa ushirikiano na International Service for the Acquisition of Agri-biotech Applications (ISAAA) AfriCenter na NBA katika Chuo Kikuu cha Embu wiki iliyopita, kongamano hilo lililenga kuleta pamoja wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini vinavyotoa mafunzo ya kilimo na wadauhusika katika bunifu za bayoteknolojia.
Joseph anaendeleza kilimo cha pamba ya kisasa katika wadi ya Nyangati, Kirinyaga.
Mkulima mwingine, Evans Ngure analalamikia jitihada zake kukuza pamba nusra zisambaratishwe na kero ya mbegu kufikia wakulima zikiwa zimechelewa.
“Kwa mfano, msimu wa upanzi 2023 (Oktoba – mvua ya msimu mfupi) mbegu ziliwasili mwezi mmoja baada ya kipindi ambacho zinapaswa kuwa udongoni,” Ngure anaelezea.
Pamba inalimwa misimu miwili kwa mwaka; mvua kubwa – Aprili na ule wa mvua kiduchu – Oktoba.
Kenya huagiza mbegu za pamba iliyoboreshwa kutoka India.
Joseph Thika amekuwa katika kilimo cha zao hilo tangu miaka ya tisini (1990’s), na anakiri pamba ya kisasa ina mapato.
Awali, alikuwa akikuza ile asilia (conventional) ambayo inahangaishwa kwa kiwango kikubwa na mdudu aina ya boll warm na aphid.
“Bt cotton imeimarishwa kiasi kuwa inahimili athari za wadudu, hasa, yule mharibu zaidi; African boll worm,” Dkt Paul Chege, mtaalamu kutoka ISAAA anasema.
Isitoshe, afisa huyu anasifia pamba hii ya kileo idadi ya kupulizia dawa dhidi ya wadudu na magonjwa imepungua kutoka mara kumi na mbili kwa msimu hadi wastani wa tatu pekee.
“Kando na kuhimili mikumbo ya athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile mkurupuko wa wadudu, magonjwa ya mimea na kiangazi, inasaidia kudumisha usalama wa mazingira kwa sababu ya punguzo la kiwango cha kupulizia dawa,” anafafanua Dkt Chege.
Wakulima wa pamba Kirinyaga, mazao yao hununuliwa na Meru Ginnery – kiwanda, Joseph akidokeza kwamba kilo moja bei huuza Sh72.
Chini ya vigezo faafu kitaalamu, hekta moja inazalisha wastani wa tani 1.5 za pamba iliyoboreshwa ikilinganishwa na kati ya kilo 400 na 600 ile ya zamani.