Uamuzi wa Jumwa na Dori kutimuliwa ODM wakaribia
NA WAANDISHI WETU
HATIMA ya Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na mwenzake wa Msambweni Suleiman Dori itajulikana karibuni wakati wabunge hao watafika mbele ya baraza kuu la chama cha ODM.
Mwaka 2018 katika mkutano ulioongozwa na Kinara wa ODM, Raila Odinga, chama hicho kiliidhinisha mapendekezo ya kuwatimua Bi Jumwa na Bw Dori pamoja na wawakilishi wengine saba wa wadi.
Uasi wa wabunge hao umeanza kuwachimbia katika maeneo yao ya uwakilishi baada ya makundi na viongozi wengine wa ODM kuwataka wajiuzulu ili uchaguzi mdogo uandaliwe.
Jumapili, wanachama wa kundi la Ngumu Tupu linaloegemea upande wa ODM katika kaunti ya Kwale, walimuonya vikali Bi Jumwa dhidi ya kumhusisha Gavana Hassan Joho wa Mombasa katika masaibu yanayomkumba ndani ya ODM.
Hii inafuatia kauli aliyotoa mbunge huyo wiki jana kwamba Bw Joho ndiye anayedhamini mipango ya kumtimua chamani.
Mnamo Jumamosi, Bi Jumwa alikataa kumjibu mbunge wa Likoni Mishi Mboko, rafikiye wa zamani ambaye sasa ni hasidi wake akisema analenga kumenyana na gavana moja kwa moja.
Bi mboko alikuwa amemshutumu vikali kwa kumhusisha gavana huyo na yanayomkumba katikaODM.Bi Jumwa hata hivyo amekuwa akisisitiza kwamba ana mkataba wa hadi mwaka wa 2022 na ODM, na wakati huo ndipo atakapogura na kujiunga na kambi ya Naibu Rais William Ruto.
Mwenyekiti wa kundi la Ngumu Tupu, Hassan Chitembe alisema kwamba tayari wamemteua Idd Omar Boga kuwania kiti cha eneobunge la Malindi iwapo uchaguzi mdogo utaandaliwa huku akimtaka Bi Jumwa kukoma kumhusisha Bw Joho na masaibu yake.
Mbunge wa Ganze, Teddy Mwambire ambaye alikuwa mwenyeji wa Bw Odinga wakati wa mkutano na madiwani wa eneo hilo naye alieleza Taifa Leo kwamba ‘ukaidi’ wa Bi Jumwa na Bw Dori haukujadiliwa wakati wa mkutano huo.
“Hatukujadili misimamo ya wawili hao. Tulijadili tu masuala ya maendeleo yanayohusu Kaunti ya Kilifi,” akasema Bw Mwambire.