Habari za Kitaifa

Afisa wa DCI aagizwa amrudishie Rashid Echesa Sh200, 000 alizomnyang’anya


AFISA wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) ameagizwa na mahakama amrudishie mara moja aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa Sh200,000 alizotwaa kutoka kwake wakati wa uchunguzi wa madai ya kujiteka nyara kwake na malumbano kati yake na Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa.

Afisa huyo Kenneth Bowen aliagizwa na Hakimu Ann Mwangi amrudishie Bw Echesa pesa zake katika muda wa siku 14.

Endapo Bowen hatamrudishia pesa hizo, sheria itachukua mkondo wake na ataona cha mtema kuni.

Echesa alinyang’anywa pesa hizo Machi 18, 2024 alipoenda kituo cha polisi cha Karen akidai alikuwa ametekwa nyara na kuteswa.

Hakimu alitoa agizo hilo baada ya kuelezwa na afisa mwingine wa afisi ya DCI kwamba pesa hizo hazikuwasilishwa katika makao makuu ya DCI kama alivyodai Bowen.

Awali, Bowen alikuwa ameagizwa na hakimu afike kortini kueleza alikopeleka pesa hizo alizochukua kutoka kwa Echesa alipofika katika kituo cha polisi cha Karen kupiga ripoti ya kutekwa nyara kwake na kuteswa.

Bowen alikiri kortini alizichukua kutoka kwa Echesa pamoja na simu, kisha akazipeleka kwa makao makuu ya DCI kwa uchunguzi zaidi.

“Pesa hizo Sh200,000 hazikuwasilishwa katika afisi ya DCI – Mazingira House iliyoko Kiambu Road,” afisa anayechunguza kesi ya Waziri huyo wa zamani na Gavana Barasa alieleza mahakama.

“Ni wewe ulitwaa pesa za Echesa. Mrudishie katika muda wa siku 14 la sivyo sheria itakuandama,” Bi Mwangi alimweleza Bowen.

Echesa na washukiwa wengine walikamatwa na kushtakiwa kwa kashfa ya kudai kima cha Sh240 milioni kutoka kwa Barasa.

Vilevile, alilalamikia vitisho kutoka kwa Gavana huyo wa Kakamega.

Baada ya kushtakiwa waliachiliwa kwa dhamana.