Olunga: Hata mimi napinga mswada tata wa Fedha wa 2024
MWANASOKA Michael Olunga amekuwa mwanamichezo wa kwanza kuunga mkono vita dhidi ya Mswada tata wa Fedha wa mwaka 2024.
Olunga kutoka klabu ya Al Duhail nchini Qatar anasema yuko pamoja na Wakenya katika vita hivyo ambavyo vimeshuhudia maandamano makubwa kote nchini ya vijana wa kizazi kipya maarufu Gen Z ambao wanapinga Mswada wa Fedha 2024 ulio na mapendekezo ya ushuru utakaowaumiza.
Mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 30 ameweka bango kwenye mtandao wake wa X linalosoma kwa kimombo Reject not Amend (kataa wala si kurekebisha).
Beki wa kupanda na kushuka Erick Ouma “Marcelo” anayecheza soka ya malipo nchini Uswidi ameunga mkono nahodha wa timu ya taifa ya Harambee Stars, Olunga kwa kusema kwa kimombo Inject and reject kwa maana kuwa ongeza nguvu na kukataa.
Mmoja wa watumiaji wa mitandao ya kijamii kwa jina Mourinho’s Boya, hata hivyo, amekataza wanasoka dhidi ya kujihusisha na siasa.
Anadai kuwa sheria za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) zinawakataza wanasoka kujiingiza katika masuala ya siasa.