Vurugu waumini wakipinga pasta kutumia hela za kanisa kujinunulia gari
Na CAROLINE MUNDU
VURUGU zilitokea katika Kanisa la Nyalenda Baptist mjini Kisumu Jumapili kufuatia madai kwamba pasta alitumia pesa za kanisa kununua gari bila idhini ya waumini.
Pasta Samuel Otieno, pamoja na wasimamizi wengine wakuu wa kanisa hilo, walidaiwa kutoa Sh800,000 kwenye akaunti ya kanisa na kununua gari aina ya Toyota Axio bila ruhusa wala kufahamisha waumini na viongozi wengine.
Kulingana na katibu wa kanisa, Bi Monica Mugaro, fedha za kanisa zilitolewa benki bila yeye kujua kama inavyohitajika na kanuni za usimamizi wa kanisa hilo.
“Tulishtuka tulipofahamishwa kupitia kwa tangazo kanisani kwamba pesa zilitolewa benki na gari likanunuliwa. Zaidi ya hayo, hatujaonyeshwa risiti wala kuona pesa zilizobaki baada ya gari kununuliwa,” akasema.
Hata hivyo, Bw Otieno pamoja na Shemasi Mkuu wa kanisa, Bw Dennis Oduol walikanusha madai hayo na kuahidi kuwasilisha stakabadhi zote ambazo waumini wenye malalamishi wanataka kuona.
“Kabla Jumapili ijayo tutakuwa tayari tumewaita viongozi wenye malalamishi na kuwaonyesha kila stakabadhi za ununuzi wa gari hilo,” akasema Bw Otieno.
Duru zilisema kuwa viongozi waliouliza kuhusu fedha hizo walipewa barua kwamba wameondolewa kwenye nyadhifa zao kwa mwaka mmoja na wakaonywa wasiwahi kuingia katika uwanja wa kanisa wala kujihusisha na waumini wengine.
Mwenyekiti wa kanisa hilo alimlaumu pasta wao kwa kile alichosema ni kuwadhulumu waumini.
“Tunagharamia ada zake za maji, stima, marupurupu kila Jumapili ilhali bado anatumia vibaya fedha za kanisa. Ni wazi kwamba yeye si kiongozi anayeongozwa na roho mtakatifu,” akalalama mwenyekiti huyo, Bi Catherine Otieno.
Kioja hicho kilivutia maafisa wa polisi wenye silaha ambao waliitwa kutuliza hali.
Mapasta wamekuwa wakilaumiwa kwa kuishi maisha ya kifahari huku waumini wao wengi wakiishi maisha ya uchochole.