Chanjo za watoto zilizonunuliwa na serikali majuzi zaisha bila kufika kaunti 10
UCHUNGUZI wa Taifa Leo umebainisha kuwa angalau kaunti 10 bado hazijapokea chanjo ya watoto tangu mwaka jana.
Chanjo hizo ni za kuzuia magonjwa ya Kifua Kikuu (BCG), Polio (bOPV), Pepopunda-Dondakoo (Tetanus-Diphtheria), na ukambi na upele (Measles Rubella).
Kaunti zilizoathiriwa ni Bomet, Narok, Turkana, Wajir, Mandera, Garissa, Uasin Gishu, Marsabit, Bungoma, Kakamega, Tana River, Homabay na Isiolo.
Mapema mwaka jana, Wizara ya Afya (MoH), ilitangaza kuwa ilinunua chanjo za watoto za kima cha Sh1.25 bilioni.
“Kufikia leo, tunafurahi kutangaza kuwa tumepokea chanjo zifuatazo: dozi 1,209,500 za kuzuia maradhi ya surua na upele, dozi 3,032,000 za chanjo ya polio (ya kuwekewa mdomoni), dozi 1,000,000 za chanjo ya Pepopunda-Dondakoo na dozi 2,120,000 za chanjo ya BCG,” alisema Katibu katika Wizara ya Afya kwenye Idara ya Huduma za Afya Harry Kimtai.
Wakati huo alikuwa anahakikishia Wakenya kuwa chanjo zilizowasili wakati huo zilikuwa zinaandaliwa kwa usambazaji katika vituo 9 vya kuhifadhi chanjo kote nchini.
Wizara ya Afya ilitoa maelezo haya kuhusu shehena ya chanjo ambayo ilipokewa Kenya kutoka kitengo cha usambazaji chanjo cha Hazina ya Watoto ya Shirika la Umoja wa Mataifa (UNICEF).
Kulingana na serikali, kuchelewa huku kulisababishwa na deni la Sh1.5 bilioni kwa mashirika ya UNICEF na GAVI (shirika la kimataifa la kusambaza chanjo kwa mataifa maskini duniani) ambayo husambaza bidhaa hii muhimu.
Akizungumza na Taifa Leo, Bw John Kibet, baba wa mtoto ambaye bado hajapokea chanjo, alisema amekuwa akitembelea zahanati kadhaa kaunti ya Bomet akitafuta chanjo bila mafanikio.
Baba atafutia mwanawe chanjo Bomet bila mafanikio
“Mtoto wangu alizaliwa Disemba 17, 2023. Kituo hicho cha afya kilisema hakina chanjo ya BCG. Imepita miezi sita sasa na bado mtoto wangu hajapokea chanjo. Juni mwaka huu, alipohitimu miezi 6, tulienda kutafuta chanjo ya Rotavirus ya kuzuia kuendesha kwa matumaini ya kupata ile ya BCG baada ya serikali kusema imenunua chanjo, lakini hatukupata kitu,” aliambia Taifa Leo.
“Tulitembelea vituo kadhaa vya afya jana usiku kaunti ya Bomet na bado tulikosa chanjo,” aliongeza.
Katika eneo la Saku, Kaunti ya Marsabit, Bi Halima Abdi, mwenye umri wa miaka 38, alijifungua miezi minane iliyopita.
“Nimetoka katika zahanati ya Badassa. Hakuna chanjo ya kumpa mtoto wangu; tumeambiwa tungoje hadi watakapotuambia,” aliambia Taifa Leo huku akifichua kuwa alisafiri hadi katika vituo vya afya vya Laisamis na North Horr akaambulia patupu.
“Bado mtoto wangu hajapata chanjo; nimekata tamaa,” Halima ambaye ni mama wa watoto wawili, alilalama.
Huko Shikokho, Kakamega Kusini, Kaunti ya Kakamega, Bi Mary Nabutola alieleza kuwa mtoto wake wa miezi saba ni miongoni mwa wale ambao bado hawajapokea dozi yoyote ya chanjo ya utotoni.
Mama huyu wa watoto watatu alieleza kuwa alienda katika Hospitali Kuu ya Kaunti ya Kakamega na kuambiwa itabidi awe na subira. Bi Nabutola aliambiwa atulie hadi afahamishwe pindi chanjo zitakapowasili.
“Haya yalijiri mwezi uliopita baada ya kuzuru vituo kadhaa vya afya ambapo watoto wangu wengine walipewa chanjo, ambao sasa wamekua. Wajua, siwezi kumudu kutumia fedha barabarani nikitafuta chanjo licha ya kujua umuhimu wa chanjo kama ya BCG. Nitumie pesa kwa chakula ama nauli?” aliuliza.
Wakazi wapanga foleni wakisubiri chanjo Turkana
Katika zahanati ya Kangamojoj Turkana Kaskazini, takriban kina mama waliojifungua wanapanga foleni.
“Walifika hapa saa kumi na mbili asubuhi na wamekuwa wakitafuta chanjo kwa udi na uvumba. Tulikuwa na chanjo hizi awali lakini ziliisha miezi mitatu iliyopita,” daktari mmoja ambaye amekuwa akiwahudumia kina mama wenye watoto wadogo alisema akiomba kutotajwa.
Alieleza kuwa bado wanasubiri dozi ambazo serikali ilisema imenunua.
“Kituo hiki cha afya kinategemewa kwa chanjo na eneo pana la zaidi ya ekari 50. Kama hatuna chanjo hapa, hata vituo vingine eneo hili vinaweza kukosa,” aliambia Taifa Leo Jumatatu.
“Aghalabu sisi hutegemea maafisa wa kliniki kutoa chanjo, lakini wamekuwa katika mgomo zaidi ya miezi mitatu iliyopita. Sijui ni nani atatoa chanjo hizi zitakapowasili?” aliuliza.
Katika miongozo yake ya sera ya chanjo, wizara ya afya inaelekeza kuwa chanjo zote za sindano lazima zitolewe na matabibu waliosajiliwa ipasavyo.
Akijibu Taifa Leo katika mahojiano ya simu, Dkt Rose Jalang’o, Mkuu wa Mpango wa Kitaifa wa Chanjo (NVIP), alisema pengine kina mama wanaenda kwenye vituo ambavyo si vya kutoa huduma za chanjo.
Serikali: Pengine wanaenda vituo visivyo vya kutoa chanjo
“Nchini Kenya, tuna takriban vituo 15,000 vya afya; kati ya hivi, ni vituo 8,000 pekee hutoa huduma za chanjo. Pengine unaenda katika kituo kisichofaa kutoa chanjo kisha unasema chanjo hazijafika,” alisema.
Mkuu wa mpango wa chanjo nchini alisema amewasiliana na baadhi ya kaunti kumi zilizochunguzwa na Taifa Leo.
“Wanataka orodha ya vituo vya afya ambavyo mama hao walitembelea; kama chanjo hazijawasili, pengine ni kwa sababu havina vifaa vya kuhifadhi chanjo,” Dkt Jalang’o alisema.
Taifa Leo iliwasiliana na Waziri wa Afya Susan Nakhumicha na Katibu Hillary Kimtai ili kubaini mbivu na mbichi.
“Tuna chanjo nchini, wacha nifuatilie, Bw Kimtai alisema.
“Nitumie njia ya mawasiliano ya wazazi ambao wanatafuta chanjo,” Waziri Nakhumicha aliambia Taifa Leo.
Akijibu kauli za Dkt Jalang’o, Bi Halima alisema, “Hii si mara yangu ya kwanza kujifungua na kulea mtoto. Nimepata watoto na pia kuwapeleka kupata chanjo. Ninajua nilipopata chanjo awali; nilirejea hapo na bado sikupata. Anadhani sisi kina mama ni wajinga tukikuambia hatujafaulu kupata chanjo? Tumeunda vikundi vya WhatsApp ambapo tunaambiana sehemu za kupata bidhaa mbalimbali.”
Mmoja wa maafisa wakuu wa wizara ya afya aliambia Taifa Leo kuwa serikali ilikuwa na makataa ya hadi Julai 1 kumaliza deni la GAVI na UNICEF, ambayo yalikuwa malimbikizo ya mwaka uliopita wa kifedha.