Wanasayansi watengeneza kinywaji cha muguka wakitetea uwezo wake wa kimatibabu
WATAALAMU katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Meru (MUST) wamejitokeza kutetea mimea ya miraa na muguka, wakisema licha ya kutumiwa vibaya, ina manufaa kimatibabu na thamani kuu kiuchumi.
Wataalamu hao wametengeneza na kusajili kinywaji cha Muguka cha kuongeza nguvu ambacho kitaanza kuuzwa sokoni hivi karibuni na kinatarajiwa kutoa ushindani mkali kwa vinywaji maarufufu kama vile Red Bull.
Muguka hukuzwa kwa wingi katika maeneo kame ya Mbeere, Kaunti ya Embu huku miraa ikikuzwa katika eneo la Igembe, Kaunti ya Meru.
Jina la kisayansi kwa mmea unaozaa miraa na muguka ni Cathaedulis ambao majani na shina lake linasheheni kemikali za kulevya zinazotumika kwa burudani, tiba au mitishamba zinazofahamika kama cathinone na cathine.
Wanasayansi wawili, Profesa Joshua Arimi, ambaye ni mtaalam kuhusu chakula na Dkt Patrick Kubai ambaye ni mtafiti, wamesema tafiti zilizofanyiwa miraa na muguka zimethibitisha kuwa inasheheni viinimwili muhimu.
Wataalam hao wanasema kando na kemikali hizo mbili, miraa inasheheni kiwango cha juu cha madini muhimu na ina viambajengo vingine zaidi ya 50 ambavyo wanasayansi wanadondoa kwa lengo la kubaini manufaa yake.
“Kuhusu uongezeaji thamani, tumeunda kijifuko sawa na vile vya majani chai, kitafunio cha miraa na kinywaji cha kuongeza nguvu.
Tunafanya hivi kwa sababu miraa na muguka huchangia takriban Sh13.1 bilioni kwa uchumi wa Kenya kando na kuwa nyenzo kuu za uchumi katika maeneo inapokuzwa,” alisema Profesa Arimi.
Alizungumza Jumamosi wakati wa kufunga Kongamano la Tatu la Kimataifa la Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Meru (MUSTIC), lenye kaulimbiu, Sayansi katika Hatua ya Hali ya Anga.
“Lengo letu ni kuboresha jinsi bidhaa za muguka na miraa zinavyowasilishwa sokoni ambapo kwa sasa haivutii wateja. Hii itarahisishia mashirika ya serikali kudhibiti matumizi ya bidhaa hiyo na wanajamii ambao hawajahitimu umri,” alisema.
Dkt Kubai, aliyefanya kazi katika Hospitali ya Nyamebe Level Four kabla ya kujiunga na kundi la watafiti alisema wanaimarisha manufaa ya miraa na muguka kupitia tafiti za kimatibabu.
“Kwa mfano, utagundua watu kutoka maeneo yanayokuza miraa wanaotafuna kila siku hawaugui maradhi ya shinikizo la damu na kisukari na tumefanya udadisi kuhusu matokeo haya. Lakini hata kabla ya kuthibitisha matokeo yake ninaweza kuwahakikishia inahusu zaidi matumizi ya miraa.”
Ulaji wa muguka umezua hisia kali kutoka kaunti za pwani huku ikidaiwa wakazi wa Mombasa pekee hutumia zaidi ya Sh7 bilioni kwa mihadarati hiyo kila mwaka.