SIKU YA KISWAHILI DUNIANI: Otile Brown ajitolea kukuza talanta ya mwimbaji atumiaye Kiswahili
MWANAMUZIKI Jacob Obunga almaarufu Otile Brown amejitolea kukuza kipaji na kumnoa mtu mmoja nchini aliye na talanta ya kuimba nyimbo kwa lugha ya Kiswahili.
Otile alisema kuwa kuna haja ya wasanii kutumia lugha ya Kiswahili kwa kuimba. Alisistiza ni muhimu kufahamu lugha pamoja na lafudhi ya lugha ambayo ina ladha yake kwenye nyanja ya muziki.
“Namtafuta msanii wa kike katika nafasi ya kushauri kwenye kazi yangu. Unaweza kuwa unatoka sehemu yoyote ya Kenya mradi tu unajua kuimba Kiswahili kizuri. Lafudhi ni muhimu kwenye nyimbo zetu za Kiswahili,” alisema Otile.
Kauli za Otile zinakuja saa chache baada ya kuzindua wimbo mpya wa Kiswahili unaoitwa ‘Furukuta’.
Azimio la kuzindua wimbo huo mpya kwa lugha ya Kiswahili, ni kutambua wajibu muhimu unaotekelezwa na lugha ya Kiswahili katika kuleta amani, umoja, maendeleo ya kijamii na tofauti za utamaduni pamoja na kubuni uhamasishaji na kukuza mazungumzo miongoni mwa watu.
Mataifa ya wanachama wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA yalipitisha azimo lililowasilishwa na Kenya na Tanzania kwa niaba ya nchi za bara Afrika, kwamba Julai 7 itakuwa Siku ya Kiswahili Duniani.
“Tunatangaza Julai 7 ya kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani, itakayoadhimishwa kila mwaka kuanzia 2024,” liliamua Baraza hilo.
Kiswahili ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi zaidi duniani, ikiwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 200.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), awali liliadhimisha siku ya lugha ya Kiswahili Julai 7 kila mwaka kuanzia mwaka 2022 baada ya mkutano mkuu ulioandaliwa Novemba 23, 2021, uliotangaza Siku ya Kiswahili Duniani iadhimishwe kila mwaka.