Habari za Kitaifa

Vijana 16 wa Gen Z kusalia rumande kwa kuibia mbunge wa Kapseret

Na TITUS OMINDE July 7th, 2024 2 min read

MAHAKAMA ya Eldoret mnamo Ijumaa iliamuru vijana wapatao 16 wa Gen Z wa umri wa kati ya miaka 17 na 24 wanaokabiliwa na mashtaka ya kuiba na kuharibu mali ya thamani ya zaidi ya Sh150m katika kilabu cha Timba XO kinachohusishwa na mbunge wa Kapseret Oscar Sudi watasalia katika rumande ya gereza la Eldoret kwa takriban siku tano wakisubiri uamuzi wa dhamana.

Washtakiwa walidaiwa kuiba na kuharibu mali katika kilabu hicho mnamo Juni 25 wakati wa maandamano ya Gen Z ya kupinga ushuru katika mji wa Eldoret.

Mawakili wa utetezi walikuwa wamewasilisha ombi mahakamani kutaka washukiwa kuachiliwa kwa masharti nafuu, wakitilia mkazo kwamba wengi wao walikuwa wanafunzi wa shule za upili na vyuo kutoka taasisi mbalimbali mjini Eldoret.

“Baadhi ya washtakiwa ni wanafunzi wa shule ya upili ya Wareng, shule ya upili ya Sosiot na RVTTI, naomba mahakama hii ifikirie kuwaachilia kwa dhamana,” wakili Omolo Asseso anayewakilisha mshtakiwa aliambia mahakama.

Kufuatia ombi la mawakili kuhusu masharti ya dhamana, Hakimu mwandamizi wa Eldoret Kesse Choronoh aliamuru maafisa wa uangalizi kuhusu tabia ya washukiwa kuwasilisha ripoti ya awali ya dhamana mahakamani ili kusaidia katika kubaini dhamana stahiki.

Bi Cheronoh alisema alisita kutoa uamuzi kuhusu bondi kabla ya kubaini hali ya washtakiwa baada ya mawakili wanaowawakilisha kudai kuwa baadhi yao walikuwa wanafunzi.

Afisa wa uangalizi ambaye alikuwa kortini aliahidi kuwa tayari na ripoti hiyo ifikapo Julai 9 kesi hiyo itakapotajwa.

Kumi na sita hao walishtakiwa kwa kuiba, kupatikana na mali iliyoibiwa na kuharibu mali ya Timba XO Club mnamo Juni 25 wakati wa maandamano mjini Eldoret.

Upande wa mashtaka uliambia mahakama kuwa washtakiwa waliiba, spika 11 za sauti, televisheni bapa, vifaa vya taa za umeme, vyakula vya aina mbalimbali, vinywaji vya aina mbalimbali vya vileo, tarakilishi vyombo vya jikoni vya aina mbalimbali, mitungi ya gesi pamoja na bidhaa nyinginezo vyenye thamani ya Sh78,896,560 mali ya Timba XO.

Vile vile walishtakiwa kwa shtaka la pili la uharibifu wa mali ambayo ni pamoja na ofisi, chumba cha kudhibiti kamera za CCTV, duka kuu la kilabu, kaunta za pombe, viti, meza na vifaa vya kielektroniki vya aina mbalimbali vyote vikiwa na thamani ya Sh80,000,000.

Kesi hiyo itatajwa Julai 9.