Habari za Kitaifa

Sapit awataka vijana wachukue majukumu kanisani kama kwaya, wanapopigania mageuzi

Na VICTOR RABALLA July 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KIONGOZI wa Kanisa la Kianglikana Nchini (ACK) Askofu Jackson Ole Sapit sasa anawataka vijana maarufu kama Gen Z kuchukua majukumu muhimu kanisani wanapopigania mabadiliko ya nchi.

Askofu Ole Sapit Jumapili alisema wito wa vijana kufika kanisani haufai kuwa ule wa kuwazomea wanasiasa ila kutafakari jinsi ambavyo taifa lilifikia hali yake ya sasa.

“Si wakati wa kuzungumza sana bali ni wakati wa kujiuliza jinsi ambavyo tulikosea na kujipata kwenye changamoto za sasa,” akasema.

Mkuu huyo wa ACK alisema njia bora ya vijana kuingia kanisani ni kuwa wanachama kisha kujiunga na makundi ya uimbaji, kwaya na kushiriki ibada.

“Tafadhali fikeni kanisani ili Mungu atuunganishe pamoja. Bila Mungu kile ambacho mnakipigania hamtakipata na mtakuwa mkipoteza wakati bure,” akasema Askofu Ole Sapit.

Alikuwa akiongea Jumapili katika kanisa la ACK la St Peters Cathedral Ahero eneobunge la Nyando ambapo alieleza kuwa mageuzi yanayopiganiwa na Gen Z yatatimia.

“Kwa kipindi kirefu nilikuwa napigana na kuwakataza wanasiasa wasitumie eneo la kuabudu kucheza siasa. Sasa hilo ni rahisi kwa sababu vijana wetu wananiunga mkono,” akaongeza.