Habari za Kitaifa

Presha ya Gen Z yazaa matunda, Ruto akitia saini mswada wa IEBC

Na KEVIN CHERUIYOT, BENSON MATHEKA July 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto atia saini Mswada wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (uliorekebishwa)  wa 2024 kuwa sheria.

Dkt Ruto alitia saini mswada huo Jumanne katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kenyatta (KICC) jijini Nairobi mbele ya viongozi wa upinzani Raila Odinga (Orange Democratic Movement), Kalonzo Musyoka (Wiper Party), Naibu Rais Rigathi Gachagua na viongozi wa Bunge la Kitaifa na Seneti.

Hatua hiyo sasa inapisha rasmi uteuzi wa jopo la uteuzi litakaloajiri makamishna wapya wa tume ya uchaguzi.

Rais William Ruto akihutubu baada ya kutia saini mswada wa kuteua makamishna wa IEBC. Picha|PSC

Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed mnamo Jumatatu alisema mswada wa IEBC ulikuwa wa kwanza kushughulikiwa na Bunge kulingana na mapendekezo ya ripoti ya Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (Nadco).

Ripoti hiyo ni zao la kamati ya pande mbili, iliyojumuisha viongozi kutoka mrengo wa Kenya Kwanza wa Rais Ruto na Azimio la Umoja One Kenya Coalition wa Bw Odinga.

Mswada huo wa IEBC ulikuwa mojawapo ya masuala  yaliyotawala mjadala wakati wa maandamano ya hivi majuzi dhidi ya serikali, huku vijana wakitaka tume ya uchaguzi iundwe ili kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Bw Odinga alisema changamoto mpya iliyopo nchini kwa sasa inayochochewa na matakwa ya vijana wa kizazi kipya pamoja na raia kwa ujumka, inahitaji viongozi kutoa mwelekeo wa jinsi Kenya inapaswa kusonga mbele.

Alisema sheria hiyo mpya ya IEBC iliyotiwa saini italeta mabadiliko katika tume hiyo ambayo shughuli zake zililemazwa na ukosefu wa mwenyekiti na makamishna.

Aliongeza kuwa kushughulikia masuala yaliyoibuliwa na wananchi kunaweza kusaidia kumaliza maandamano yanayoendelea na akamuomba Rais kufanya mazungumzo na wadau wote.

Raila asisitiza mengi ya masuala ya vijana yapo katika ripoti ya Nadco

“Mswada huu ambao umetiwa saini kuwa sheria leo ni mojawapo tu ya masuala hayo. Masuala mengi ambayo yanaibuliwa na vijana yameshughulikiwa katika ripoti ya Nadco,” Bw Odinga alisema.

“Kenya inastahili ina kila haki ya uongozi bora. Tatizo la ukosefu wa ajira, changamoto za ubaguzi, ufisadi, ubaguzi wa kijinsia na kadhalika ni mambo ambayo yanafaa kushughulikiwa kwa dharura.”

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah ambaye alikuwa mwenyekiti mwenza wa Nadco alisema kuwa kupitishwa kwa mswada wa IEBC kunaonyesha umuhimu wa mazungumzo nchini.

Bw Ichung’wa pia alisema kwamba miswada mingine iliyotokana na mazungumzo hayo itapewa kipaumbele Bunge litakaporejelea vikao baadaye mwezi huu.

Bw Musyoka, ambaye alikuwa mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo, alisema walijiunga na serikali katika mazungumzo kwa sababu Wakenya waliibua wasiwasi baada ya uchaguzi wa 2022, ikiwa ni pamoja na madai ya wizi wa kura.

Bw Musyoka aliitaka serikali kuwasikiza vijana na kushughulikia masuala ambayo waliibua kwa dharura.