Makala

TUONGEE KIUME: Kaa ngumu dada, wanaume wanadharau mwanamke mwepesi wa kumeza chambo

Na BENSON MATHEKA July 11th, 2024 2 min read

MAFISI wapo na wataendelea kuwepo. Hawa ni wale wa kutegea viundwe wadandie, waonje kwa raha zao na kutoweka na ukicheza watakutumia na kukutema kama ganda la muwa ukiisha utamu. Kwa raha zao pia.

Wapo wanaume na wanawake walio na tabia hii na ni stadi wa kurusha mistari au kutumia pesa zao kunasa wanaomezea mate.

Kuna wale vipusa wanaoingia katika umri wa kutamaniwa. Wale warembo wabichi ambao kila mwanamume ambaye systems zake zinafanya kazi hawezi kujizuia kutamani.

 Wale ambao wanaume wanawania na hata kupigana wakiwamezea mate. Hawa ndio wale ninaozungumza nao leo. Na ninazungumza nao kama mwanamume.

Dada, ukiona wanaume wengi wanakumezea mate kwa wakati mmoja, usijifunge kwao. Usiahidi yeyote kuwa mtaoana. Usifanye hivyo. Waambie utarudi kwao. Chukua  muda ufanye chaguo bora zaidi.

Kukubali mapendekezo ya ndoa kutoka kwa wanaume tofauti ni kujiweka kwa maafa, balaa. Usifanye hivyo.

Ikiwa huna uhakika na mtu yeyote, mwambie akupe muda uwazie pendekezo au ombi lake. Hii itakufanya uwafahamu vyema wanaokurushia mistari. Ujue kama lengo lao ni kukuoa au kukutafuna na kukuacha mwa madharau.

Naam, wanaume huwa wanadharau mwanamke mwepesi wa kumeza chambo na kuingia chumbani.

 Wadadisi, wachambue wanaokupa pendekezo la ndoa, mengi ya mapendekezo huwa manukato yasiyodumu.  Lengo la kaka likiwa kuchovya, kaa ngumu. Chunguza maadili, imani, maono na matarajio ya kila kaka katika maisha na kutoka kwako.

Anayelenga ndoa atakuvumilia, anayelenga asali ataishiwa na subira na kuingia mitini ukikaaa ngumu kwa muda. Kumbuka, kabla ya kukubali pendekezo la mwanamume yeyote na kujifunga nalo, una uhuru na haki ya kujivinjari na yeyote unayetaka kwa lengo la kumjua zaidi.

Ukifanya hivi, nakupa onyo; usishawishike kuingia boksi ujipate faraghani, dada utatafunwa kabla ya kujua kilichofanyika. Nimekwambia.

Unapotoka na mwanamume, usipotoke, fahamu lengo la uchumba; sio kulishana uroda wengi wanavyodhani, kula wali wa kukaanga kwa kuku, kulamba ice cream, kutembelea ufukweni na  kuogelea  bali ni wakati wa kufahamiana na mtu. Nakuonya tena, katika kipindi hiki, usilewe, utageuka kitoweo. Pombe haina mwalimu dada.

Sote tunataka maisha ya starehe. Hakuna mtu anayetaka kuishi duniani akiteseka lakini si kila kitu kinachometa ni dhahabu na pesa sio kila kitu. Usipofushwe na pesa na ufahari zinazonunua. Maisha ya mapenzi ni zaidi ya pesa. Kwa hakika, ukiona mwanamume anayetumia pesa kama chambo, dada, fikiria mara mbili. Hata hivyo, inasikitisha, sivyo wengi wanavyofanya. Pesa mbele, wanasema heri kulilia kwa chopa kuliko kuchekea kwa vitz. Ole wako unayekwama katika kasumba hii.

Usiruhusu funguo za Harrier  anazoning’iniza mbele yako zikudanganye. Angalia vitu ambavyo havionekani kwa macho. Hekima dada, hekima.

Kwa kumalizia, chukua wakati wako na ufanye uamuzi sahihi. Hakuna mashindano katika ndoa. Hakuna tuzo kwa aliyeoa kwanza. Hakuna tuzo ya harusi bora.