Sababu zilizochangia Ruto kusaza Mudavadi akitema mawaziri wake
RAIS William Ruto alimsaza Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Mashauri ya Kigeni Musalia Mudavadi kutokana na sababu za kisiasa wala sio hadhi yake serikalini.
Tangu uhusiano kati ya Rais Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua ulipoanza kudorora mwaka jana, kiongozi wa taifa amekuwa akimvuta karibu Bw Mudavadi.
Kwa mfano, alipofanya mabadiliko ya kwanza madogo katika baraza lake la mawaziri mnamo Oktoba 23, 2023, Rais Ruto alimwongezea majukumu Bw Mudavadi kwa kumtunuku wadhifa wa Waziri wa Masuala ya Kigeni.
Awali, wadhifa huo ulikuwa ukishikiliwa na aliyekuwa Gavana wa Machakos Alfred Mutua ambaye alihamishwa hadi Wizara ya Utalii, Wanyama pori na Mali Asili.
Kulingana na mchangunuzi wa masuala ya kisiasa na uongozi, Barasa Nyukuri, kando na sababu zake za kisiasa ndani ya Kenya Kwanza, Rais Ruto pia amemdumisha Bw Mudavadi kwa sababu yeye ni kiungo muhimu katika mipango ya kushirikishwa kwa mrengo wa Raila Odinga katika serikali ya muungano anayopania kuunda.
“Isitoshe, Bw Mudavadi ni kiungo kikuu katika mchakato wa serikali ya Ruto wa kuweka mikakati ya kuendesha kampeni za kumpigia debe Raila katika azma yake ya kuwania wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika,” anaongeza.
Bw Mudavadi ndiye waziri wa kipekee ambaye alikuwepo katika ukumbi wa KICC Nairobi, Jumanne Rais Ruto alipotia saini Mswada wa Marekebisho ya Sheria Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itakayotoa nafasi ya kuteuliwa kwa makamishna wapya wa tume hiyo.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Bw Odinga, Kalonzo Musyoka pamoja na viongozi wengine wa mrengo wa Azimio.
Kulingana na Katiba, Rais hana mamlaka ya kumpiga kalamu Naibu Rais. Hii ni kwa sababu wote wawili walichaguliwa kwa tiketi moja.
Naibu Rais anaweza tu kuondoka afisini akijiuzulu au kupitia kura ya kutokuwa na imani naye itakayopitishwa bungeni.