Mudavadi hawezi kuwa msemaji wa Abaluhya – Oparanya
Na SHABAN MAKOKHA
VITA vya ubabe katika jamii ya Waluhya vimepamba moto huku naibu kiongozi wa chama cha ODM Wycliffe Oparanya akimenyana na kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi.
Bw Oparanya, ambaye ni Gavana wa Kakamega, jana alijiunga na viongozi wa eneo la magharibi kupuuza kuidhinishwa kwa Bw Mudavadi kuwa kiongozi wa jamii ya Waluhya, wadhifa aliotawazwa kushikilia 2017 katika uwanja wa Bukhungu.
Mnamo Jumamosi, Katibu Mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi (Cotu), Francis Atwoli, ambaye kwa miaka mingi amekuwa akijaribu kuunganisha jamii ya Waluhya, alikariri kuwa Bw Mudavadi ndiye msemajii wa Waluhya.
Lakini Bw Oparanya alisema msemaji wa jamii hawezi kutawazwa na mtu binafsi: “Ikiwa tunapaswa kuwa na msemaji, basi anapaswa kutambuliwa na wakazi wa jamii ambao wataeleza imani yao kwa kiongozi kama huyo,” alisema Bw Oparanya.
Akizungumza katika kijiji cha Shifuyo, Mumias Mashariki mnamo Jumapili kwenye mazishi ya Mwanarusi Oteng’o, Bw Oparanya alipuuza wito wa muungano wa Waluhya akisema hautakuwa na umuhimu wowote ikiwa lengo lake ni kuidhinisha mtu kuwa kiongozi wa jamii.
Alisema jamii hiyo imekuwa ikitajwa kama ya watu waoga, wasioweza kufanya maamuzi na iliyogawanyika kwa sababu ya ukosefu wa umoja.
“Tunafaa kuwa na mpangilio ambapo kila mtu atashirikishwa kuamua kiongozi wa jamii. Hatuwezi kukubali kiongozi ambaye amekwama mahali pamoja kwa muda mrefu. Anapaswa kuondoka apishe wengine,” alisema Bw Oparanya.
Bw Oparanya ambaye ametangaza azma ya kugombea urais 2022, alisema Bw Mudavadi ameshindwa kuongoza jamii hiyo na anafaa kupisha viongozi wengine kuchukua usukani.
“Sitabadilisha azma yangu ya kugombea urais 2022 kwa sababu mtu ambaye ameshindwa kusonga mbele ananizuia kama kiongozi wa Waluhya. Kila mmoja anafaa kupatiwa nafasi ya kujaribu bahati yake. Pengine nafasi ya Mluhya kuwa rais iko kwangu,” aliwaambia waombolezaji.
Bw Oparanya alisema Bw Mudavadi hana ujasiri wa kuongoza jamii.
Maoni kama hayo yalitolewa na seneta wa Bungoma Moses Wetangula aliyesema Bw Atwoli hafai kuchagua msemaji kwa niaba ya jamii.