Habari za Kitaifa

Kitita cha pesa za kiinua mgongo kinachosubiri mawaziri waliofutwa

Na VICTOR RABALLA July 13th, 2024 2 min read

WALIPA ushuru watabebeshwa mzigo wa Sh77.1 milioni kama malipo kwa mawaziri 20 waliopigwa kalamu na Rais William Ruto Alhamisi.

Watapokea pesa hizo kama malipo ya kuondoka afisi ambayo ni asilimia 31 ya malipo yao ya pensheni ya kila mwaka; kwa miezi 19 waliohudumu afisini.

Baada ya mawaziri hao kuidhinishwa na wabunge mnamo Jumatano Oktoba 26, 2022 Rais Ruto aliteua rasmi kupitia tangazo kwenye gazeti rasmi la serikali mnamo Alhamisi Oktoba 27, 2022.

Baada ya kuingia afisini, mawaziri hao walianza kupokea mshahara wa Sh924 milioni kwa mwaka huku mshahara wao halisi ukiwa Sh554, 400 kwa mwezi kulingana na mwongozo wa mishahara uliotolewa na Tume ya Kukadiria Mishahara ya Watumishi wa Umma (SRC).

Chini ya mwongozo huo, mawaziri walioanza kazi Novemba 1, 2022 walianza kupokea mshahara halisi wa Sh554,400, kila mmoja, kila mwezi hadi Juni 30, 2023.

Ndani ya miezi minane, mawaziri hao 22 walipokea jumla ya Sh18.3 milioni kama mshahara.

Hata hivyo, kuanzia Julai 2023 hadi Juni 30, 2024, SRC iliongeza mshahara wa maafisa wa serikali katika Serikali ya Kitaifa na hivyo kuchangia Mawaziri kuanza kupokea mshahara wa Sh957,000 kila mmoja kila mwezi.

Ikizingatiwa kuwa malipo ya kuondoka afisini hulipwa kwa kiwango cha asilimia 31 ya malipo ya pensheni kwa kipindi ambacho mtu alihudumu, mshahara wao halisi wa Sh594,000 kwa muda wa miezi 11 unatimu Sh37.1 milioni kabla ya makato kutolewa.

Hii ina maana kuwa kila waziri aliyefutwa kazi atalipwa Sh2.8 milioni kabla ya kukatwa asilimia 30, ya kawaida, na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA).

Kwa hivyo, kila waziri atalipwa Sh2.03 milioni kufuatia hatua ya Rais Ruto kuwafuta kazi mnamo Julai 11, 2024.

Walipa ushuru pia wanatarajiwa kubebeshwa mzigo mwingine baada ya Rais kutangaza kupunguzwa kwa washauri wa mawaziri kwa kima cha asilimia 50.

Kwenye taarifa kwa mawaziri hao wanaoondoka, Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei aliwaamuru wote 22 kuwasilisha orodha ya washauri wao kwa Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) kufikia Alhamisi Julai 11, 2024 jioni.

“Kwa hivyo, unashauriwa kukagua hitaji la afisi yako na utaje mashauri ambaye ungetaka kumdumisha ili akusaidie kutekeleza majukumu ya afisi yako,” akasema kwenye taarifa hiyo ambayo nakala yake ilitumwa kwa Mwanasheria Mkuu.

“Mshauri yeyote zaidi ya idadi hitajika ataondolewa mara moja kutoka utumishi wa umma,” Bw Koskei akaongeza.

Mkuu huyo wa utumishi wa umma alieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa serikali wa kupunguza matumizi ya fedha serikalini na kuimarisha utendakazi wake.