Habari za Kitaifa

Uvundo, hasira miili zaidi ikitolewa kwenye timbo la kina kirefu Pipeline

Na WAANDISHI WETU July 14th, 2024 2 min read

UVUNDO wa kuogofya ulioenea baada ya miili mitano kutolewa katika timbo, mtaani Mukuru kwa Njenga, Nairobi, ulichemsha wakazi waliokuwa wakishuhudia shughuli hiyo.

Ilikuwa siku ya pili ya uopoaji na miili yote ya waathiriwa ilikuwa imewekwa kwenye magunia yaliyofungwa kwa njia sawa kuonyesha kuwa waliuawa kwa kukatwa katwa au miili yao ilikatwa katwa na kuwekwa kwenye magunia kabla ya kutupwa kwenye timbo hilo lililoacha kutumiwa.

Miili mitano iliyoopolewa Jumamosi ilifikisha 11 idadi ya iliyopatikana katika timbo hilo tangu Ijumaa ambapo, kulingana na polisi, 6 ilipatikana huku maswali yakiulizwa kuhusu ni nani aliyetekeleza mauaji hayo ya kikatili, chanzo cha kuwaua na eneo walilouliwa.

Hii ni baada ya Rais William Ruto kusisitiza kuwa, hangekubali mauaji ya kiholela chini ya utawala wake.

Jana, kiongozi wa nchi aliagiza uchunguzi kuhusu mauaji hayo.

Kinaya ni kuwa, maiti hizo zilipatikana karibu na kituo cha polisi. Wakazi wa eneo hilo walisema hawakuwa wameripoti visa vya watu kutoweka.

Wananchi, viongozi wa kisiasa na mashirika ya kutetea haki za binadamu wanataka serikali ya Kenya Kwanza iwajibike na kueleza ni nani alitekeleza unyama huo.

Baadhi ya miili iliyokuwa ikitolewa kwenye timbo hilo ilikuwa imeanza kuoza huku ikiwa imefungwa kwa kamba. Kufikia jana, maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na kikosi cha Recce walifika kwenye eneo la tukio ili kusaidia katika kuitoa mili hiyo.

Wakazi walizua fujo miili hiyo ilipokuwa ikiwekwa kwenye mifuko ya wafu wakitaka ifunguliwe. Polisi walilazimika kufyatua vitoa machozi na risasi hewani kutawanya umati uliokuwa ukishuhudia shughuli hiyo ya kutisha huku ikidaiwa waathiriwa walikuwa wanawake wa umri mdogo.

Maafisa wa kikosi cha upelelezi wa jinai wakikagua miili iliyopatikana katika timbo la Kware, eneo la Mukuru Kwa Njenga, Embakasi. Picha|Bonface Bogita

Usalama pia uliimarishwa katika mochari ya City ambako miili ilipelekwa na maafisa wa kikosi cha Recce kuhifadhiwa. Mkuu wa DCI, Mohamed Amin, alithibitisha kwamba, wapelelezi walikuwa wakichambua sampuli kutoka eneo la tukio ili kubaini kilichotokea.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa waathiriwa hao wote waliuawa kwa njia moja. Miili yao imepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City Mortuary, ambako inasubiri kufanyiwa upasuaji,” Bw Amin alisema.

Kiongozi wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga, alisema serikali inafaa kuwajibika kuhusiana na vifo hivyo.

“Ni wakati wa huzuni nchini. Yale ambayo tumeshuhudia eneo la Mukuru Kwa Njenga, yananitia uchungu sana. Ninatuma rambirambi zangu kwa familia zilizopoteza wapendwa wao. Wahusika wa vitendo hivi na vingine viovu lazima wachukuliwe hatua mara moja. Wananchi wanataka uwajibikaji,” alisema Bw Odinga kwenye mtandao wake wa kijamii wa X (Twitter).

Tume ya Taifa ya Haki za Kibinadamu (KNHRC) iliitaka serikali ya Rais William Ruto kufichua ukweli kuhusu vifo hivyo.

“Baadhi ya miili iliyotolewa kwenye timbo moja huko eneo la Mukuru, Embakasi Kusini, ilikuwa imekatwakatwa. Utawala wa Kenya Kwanza, chini ya Rais William Ruto lazima uwajibike kwa uhalifu huu wa kutisha,” tume hiyo ilisema.

Wakazi wa eneo hilo wanalalamikia kuzorota kwa usalama ikiwemo ongezeko la visa vya watu kujitia kitanzi kiholela. Aidha, wamelaumu polisi kwa utepetevu na kukosa kuchukua hatua kwa wakati ufaao, hali iliyowafanya raia kuchukua hatua mikononi mwao na kuwateketeza washukiwa watatu wa wizi hivi majuzi.

Uvumbuzi huo sasa umechemsha ghadhabu ya Wakenya waliokuwa wametulia hasa baada ya Rais William Ruto kuwatimua mawaziri wake wote Alhamisi.

Inashukiwa kuwa, miili hiyo ni ya watu waliouawa na polisi wakati wa maandamano katika eneo la Githurai na Rongai, Nairobi, kabla ya kutupwa eneo hilo.

Visa vya watu kutekwa nyara na kupatikana baadaye wakiwa wameuawa kikatili vimeongezeka mno katika siku za hivi karibuni, baadhi yao wakiwa wale waliotekwa kufuatia maandamano ya kupinga serikali kote nchini yaliyoendeshwa na vijana.

Na MILLICENT MWOLOLO, WINNIE ONYANDO na BARBANAS BII