Habari Mseto

Wanafunzi 25 wakimbizwa hospitalini kufuatia ajali ya basi lao wakielekea kwa tamasha


WANAFUNZI 25 kutoka Shule ya Upili ya St Joseph’s Kemasare na ile ya Nyameru katika Kaunti ya Nyamira walikimbizwa hospitalini Jumapili asubuhi baada ya basi walimokuwa wakisafiria kupata ajali.

Basi hilo linasemekana kupoteza mwelekeo na kugonga nyumba moja eneo la Senta, karibu na soko la Miruka mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi.

Wanafunzi hao walikuwa wakisafiri kuelekea Kisumu kwa tamasha za muziki za kanda ya Ziwa wakati kisa hicho cha kusikitisha kilipotokea.

Kulingana na Dkt Donald Mogoi, Waziri wa Afya wa Nyamira, basi hilo lilikuwa limebeba wanafunzi 43 na walimu sita.

Wakati wanafunzi 18 na walimu 5 hawakupata majeraha yoyote, wengine walilazwa katika kituo hicho wakiwa na majeraha ya tishu laini ambayo yalihudumiwa na matabibu.

“Wanafunzi 25 na mwalimu mmoja wana majeraha ya tishu laini. Wengine watalazimika kuchunguzwa kwa kufanyiwa CT scan ili kujua kiwango cha majeraha. Tutawalaza wale ambao watahitaji matibabu zaidi,” Dkt Mogoi alisema.

Waziri huyo aliongeza kuwa hospitali hiyo ilitoa ushauri nasaha kwa wale ambao walitoka bila kujeruhiwa kabla ya kuwaruhusu waende makwao.

Waliposikia kwamba watoto wao walikuwa wamehusika kwenye ajali, wazazi walimiminika katika kituo hicho kuwaangalia.

Mbunge wa Mugirango Magharibi Steve Mogaka alikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza waliotakia wanafunzi walioathiriwa afueni ya haraka. Shule hizo zinatoka katika eneobunge lake.

“Tunawatakia afueni ya haraka madaktari wetu hospitalini wanapowahudumia,” Bw Mogaka alisema.

[email protected]