Habari za Kaunti

Hasara wanafunzi wenye ghadhabu wakiteketeza bweni

Na GEORGE MUNENE July 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MALI ya mamilioni ya pesa jana iliharibiwa kutokana na moto mkubwa uliotokea katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Karia, Kaunti ya Kirinyaga.

Tukio hilo la Jumapili, Julai 14, 2024 usiku lilivuruga shughuli katika shule hiyo ambayo ipo kilomita chache kutoka mji wa Kerugoya.

Moto huo uliteketeza bweni ambalo lilikuwa likisitiri wanafunzi 100 japo hakuna mtu yeyote ambaye alijeruhiwa.

Inadaiwa kuwa wanafunzi ndio waliteketeza bweni hilo kwa kile kinachodaiwa kuwa hofu ya mtihani. Juhudi za wazimamoto kutoka kaunti kuuzima moto huo zilipigwa breki na wanafunzi ambao waliwatimua.

“Tulipofika shuleni, wanafunzi waliturushia mawe. Pia waliharibu dirisha la gari la zima moto,” akasema John Kiama mmoja wa maafisa wa kaunti.

Wanafunzi hao walianza kuzua vurugu saa nne asubuhi kabla ya moto huo kuanza ndani ya bweni na kuteketeza magodoro, vitanda, nguo na vitu vingine.

Ilibidi polisi wa kupambana na ghasia (GSU) wafike na kurejesha utulivu shuleni humo.

“Hata walimu hawakusazwa kwa sababu baadhi yao walitimka mbio huku wanafunzi wakiwarushia mawe. Ilitulazimu kuwaita maafisa wa polisi kurejesha utulivu,” akasema Bw Kiama.

Tukio hilo linajiri siku moja tu baada ya bweni jingine katika Shule ya Upili ya Kerugoya kuteketezwa na wanafunzi. Kutokana na kisa hicho, shule hiyo ilifungwa na wanafunzi wakatumwa nyumbani.

Kamishina wa Kaunti ya Kirinyaga Hussein Allasaw alilaani matukio hayo mawili na kuwaonya waliohusika kuwa watakamatwa.

“Tunaendelea kuchunguza visa hivyo na waliohusika watakamatwa,” akasema.