Muungano wa kina mama ulivyozaa kampuni ya kuchinja kuku
UMOJA ni nguvu utengano ni udhaifu, hii ndiyo kauli ya muungano mmoja wa kina mama katika Kaunti ya Makueni ambao ushirikiano wao wa kujiendeleza kimaisha ulizalisha kampuni ya kukuza na kuchinja kuku.
Global Organic Chicken Ltd, kampuni iliyoanza kukita mizizi zaidi ya miaka 10 iliyopita inashirikisha wakulima wanaofuga kuku halisi wa kienyeji na walioboreshwa.
Simulizi yake ni sawa na mtoto anavyozaliwa, kukua hadi akawa mtu wa manufaa kwenye jamii licha ya changamoto za hapa na pale zisizokosa.
Shirika hilo kwa sasa likiwa linavuma si tu katika kaunti mwenyeji, ila pia Nairobi, Kitui na Taita Taveta, Eunice Musyoka ndiye Mwasisi na Mkurugenzi Mkuu.
Eunice, alikuwa mama wa nyumbani ambaye majukumu yake yalikuwa kulea watoto na kuwashughulikia.
“Kama mama, nilitafakari kuhusu biashara ambayo ningeanzisha, isiyo na ushindani mkuu na ambayo ingenisaidia kukidhi mahitaji ya familia yangu ya kimsingi bila kutegemea mume,” anasema.
Huo ulikuwa mwaka wa 2012 wazo hilo lilipomtinga.
Kulingana na Eunice, jawabu la kitendawili hicho likawa kuingilia ufugaji wa kuku.
Anadokeza kwamba alianza na kuku 10, mwaka mmoja baadaye, 2013, akajipata akifanya mauzo ya zaidi ya 400.
“Nilitia kibindoni kima cha Sh144, 000, mapato ambayo yalinichochea kushawishi wanawake wenzangu kijijini,” aelezea mfugaji huyo.
Alifanikiwa kushawishi kina mama wawili kuanzisha kundi la kijamii mashinani (Self-Help Group) ambalo kufikia 2018 lilistawi na kuwa kampuni, Global Organic Chicken Ltd.
Usajili wa kampuni hiyo yenye hisa, uligharimu Sh30, 000.
“Tulianza kwa kuandikisha wanawake 10 na kufikia 2022, idadi ilikuwa imegonga 4, 000.”
Hutoa mafunzo ya ufugaji bora, kusambazia memba vifaranga, malisho na chanjo, wakifikisha umri wa miezi mitatu au minne, shirika hilo linawanunua na kuwatafutia soko.
Huku mafunzo yakitolewa kwa makundi ya kina mama 15 hadi 30, wanapofuzu hupewa cheti.
Miaka 11 baadaye, Eunice ana kila sababu ya kutabasamu kufuatia hatua walizopiga kimaendeleo.
Eneo la Kilala, Wote, Kaunti ya Makueni, Global Organic inajivunia kuwa na kiwanda cha kisasa kuchinja kuku na kusaka soko lenye ushindani mkuu.
Mkabala mwa barabara inayoingia Mjini Makueni, ndiko kiwanda hicho kilipo.
Aidha, kina mitambo ya kisasa ya kuchinja, kutoa manyoya, kupakia na kuhifadhi.
Mazingira yakiwa yanayodhibitiwa, kina uwezo wa kuchinja kuku 1, 200 kwa siku, Eunice akisema uwekezaji huo unatokana na akiba yao kupitia uuzaji wa mashamba waliyokuwa wamenunua.
Isitoshe, walipata usaidizi kupitia shirika la United States Agency for International Development (USAID) chini ya mpango wake wa Kenya Crops and Dairy Market Systems (KCDMS), uliolenga kupiga jeki wakulima kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.
Mradi huo, hata hivyo, ulitamatika mwaka uliopita, 2023.
USAID pia imewafaa pakubwa katika utoaji mafunzo ya ufugaji bora na faafu wa kuku.
Kufikia sasa, Global Organic Chicken Ltd inahudumu na wakulima wasiopungua 8, 000.
Kando na Makueni, imeandikisha wafugaji kutoka Kitui na Taita Taveta.
Kila awamu mkulima hupata vifaranga 100 na tunahakikisha tunafuatilia wanavyofugwa, Eunice anafichua, akiongeza kuwa hushirikiana kwa karibu na kampuni tajika na aminifu za kuangua vifaranga.
Kampuni hii imenogesha soko jijini Nairobi, hasa kwenye mikahawa na eneo la Makueni, kuku mwenye wastani wa kilo 2 hadi 3, mfugaji akitia mfukoni Sh700.
“Nasi, tunapowaongeza thamani kwa kuwachinja na kuwapakia, kilo moja inachezea Sh600,” Eunice akasema wakati wa mahojiano.
Eunice alidokeza kwamba yeye hufuga idadi ya kuku kati ya 1,500 hadi 2,000.
Licha ya safari yake ya kusisimua na kuridhisha kuinua kina mama katika jamii, anasema gharama ya chakula cha madukani, usafirishaji kuku kutoka kwa wakulima na ada zinazotozwa kwenye mipaka ya kaunti (cess), inatishia jitihada za Global Organic.
Kwa wanawake wenza, mama huyu mcheshi na jasiri anawahimiza kuingilia ufugaji, simulizi yake ikiashiria biashara yenye mashiko.