Gen Z wa Lamu wakataa kupiga sherehe, wataka mamilioni ya Tamasha za Utamaduni yafutwe
VIJANA wa kizazi cha Gen Z Lamu wametoa ilani ya siku saba kwa serikali ya kaunti hiyo kutimiza kwa lazima matakwa zaidi ya kumi yanayofungamana na matumizi ya fedha za umma.
Gen Z hao wanaishinikiza serikali ya Kaunti ya Lamu kufutilia mbali mamilioni ya fedha ambayo yamekuwa yakitumika kila mwaka kufadhili maadhimisho ya Tamasha za Utamaduni wa Lamu.
Tamasha hizo za siku nne mfululizo husherehekewa kisiwani Lamu kati ya Novemba na Desemba na kuvutia maelfu ya wenyeji, wageni na watalii kutoka pande zote za Lamu, Kenya na ulimwengu.
Vijana hao pia wanashinikiza kaunti chini ya uongozi wa Gavana Issa Timamy kurejesha mara moja mfuko wa basari kwa wanafunzi wanaosoma vyuo vikuu, kufutiliwa mbali kwa bajeti ya fedha za umma zinazotumika kufadhili ziara za nje ya nchi kwa mawaziri wa serikali ya kaunti na pia Bunge la Kaunti ya Lamu.
Masharti mengine ni kuhakikisha hospitali zote za umma Lamu zinawekwa dawa za kutosha na madaktari na wauguzi wa kutosha waajiriwe.
Vile vile Gen Z wanashurutisha ukaguzi wa makampuni yote 18 ambayo yamekuwa yakiongoza katika kukabidhiwa zabuni kutoka kwa serikali ya kaunti ya Lamu ili kutoa huduma zao.
Matakwa mengine ni ukaguzi wa makundi yote ambayo yamekuwa yakinufaika na mpango wa utoaji ruzuku kutoka kwa serikali ya kaunti ya Lamu, kuondolewa kwa wafanyakazi wote wanafamilia walioajiriwa na serikali ya kaunti ya Lamu, kusitishwa kwa ukaguzi, upasishaji na uajiri wa wafanyakazi kisiasa, kupunguzwa kwa kiwango kinachotumika kulipa mishahara kutoka asilimia ya sasa ambayo ni 54 hadi 35 na kaunti kuhakikisha wakazi wote wa Lamu wanaosajiliwa kulipiwa bima ya kitaifa ya afya (NHIF) hawabaguliwi.
Gen Z wa Lamu pia wanataka maafisa wote wenye kesi za ufisadi kufuatiliwa na kuchukuliwa hatua.
Wametaja matakwa yote waliyotoa kuwa ya dharura na yasiyofaa majadiliano ya aina yoyote isipokuwa kuzingatiwa na kutimizwa kikamilifu.
“Endapo kaunti itafeli kutekeleza matakwa hayo baada ya siku saba, tuko tayari kutembea na kujazana kwenye makao makuu ya serikali ya kaunti ya Lamu mjini Mokowe ili kudai haki yetu,” ikasema notisi iliyotolewa na vijana hao.