• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Mbunge aongoza maandamano ya ‘Vuguvugu la Washenzi’

Mbunge aongoza maandamano ya ‘Vuguvugu la Washenzi’

Na PETER MBURU

MATAMSHI ya Rais Uhuru Kenyatta dhidi ya viongozi wanaomsukuma ‘kupeleka maendeleo’ katika ngome yake kuwa ni ‘washenzi’ yamezidi kuvuta hisia mseto kutoka kwa viongozi na Wakenya, huku mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri akianzisha ‘Vuguvugu la Washenzi.’

Jumanne, mbunge huyo akiandamana na kikundi cha vijana walimlaumu Rais Kenyatta kuwa amepotoka kwa kuwatusi wale waliomfanya Rais na kulaumu hali ya mambo kwa muafaka wake na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Akivalia tisheti iliyochapishwa maneno “Mimi ni mshenzi, Je wewe mwana Kenya?” mbunge huyo alifanya maandamano na kuongoza wafuasi katika nyimbo na maombi, tukio zima likiishia kumlaumu Bw Odinga kuwa ndiye ‘anampotosha mtoto wa jamii ya Mlima Kenya’.

“Tumekubali sisi ni washenzi, kwa hivyo tukasema siku ya leo tunaenda kuanzisha vuguvugu la washenzi. Kama mimi ni mshenzi, tumedanganywa na barabara, akatudanganya 2013 tutajengewa bwawa huko juu ili watu wa Bahati na Nakuru wapate maji, halikupatikana, tukiuliza kuna makosa?” mbunge huyo akauliza.

 

Siafu

Alisema kuwa Rais anaona kuwa hana haja tena na wafuasi wake, ambao katika uchaguzi uliopita walikuwa wakijiita ‘Thuraku’ (siafu) kuashiria namna wangejitokeza kwa wingi kumpigia kura, ndipo sasa anawaongelesha atakavyo.

“Wewe ni Rais wetu, shujaa wetu lakini umepotea. Usikubali kumwagia Thuraku mafuta taa ama jivu moto. Kama unasema utakuja kubadilisha katiba, ujue thuraku thuraku ndio watakusaidia,” akasema.

Baadaye, pamoja na wafuasi wake walianza kulia mbele ya kamera, huku wakiomba kwa mwenyezi Mungu na kumlaumu Bw Odinga kwa hali ya mambo

“Si kupenda, ni uchungu tunao. Raila wachana na Uhuru wetu, wachana na mtoto wetu,” wakawa wakisema wakati wa wimbo, vilio na maombi.

You can share this post!

Mbunge wa ODM amtetea Uhuru dhidi ya kejeli za wabunge wa...

Kimani Ngunjri ajificha baada ya kuzindua ‘Vuguvugu...

adminleo