Habari za Kitaifa

Watumishi wa umma waisuta SRC kwa kukatalia nyongeza yao ya mishahara

Na VICTOR RABALLA July 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WATUMISHI wa umma wamelaumu Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) kwa kuzuia, kinyume na sheria, nyongeza ya mishahara yao baada ya Mswada wa Fedha 2024 kufutiliwa mbali.

Wamekosoa vikali hatua ya SRC ya kusimamisha utekelezaji wa awamu ya pili ya nyongeza ya mishahara kuambatana na Mkataba wa Malipo (CBA) uliosajiliwa katika Korti ya Ajira na Leba.

Naibu Katibu Mwandalizi wa Muungano wa Watumishi wa Umma Nchini (UKCS) Wilson Asingo, Jumapili alisema hatua hiyo inakiuka CBA iliyoafikiwa na kamati kuu ya majadiliano.

“Huu ni mkataba uliopo na unaoendelea unaoagiza serikali kuwakinga wafanyakazi katika sekta ya umma dhidi ya gharama ya maisha inayozidi kupanda na kuboresha maisha yao,” alisema Bw Asingo.

“Tutaanza kujadiliana upya au tutaacha kilichokwisha kujadiliwa na kuafikiwa?” Alihoji akihutubia vyombo vya habari jana mjini Kisumu.

Bw Asingo alisema ushauri na maoni ya SRC yaliitishwa kabla ya CBA kusajiliwa jinsi inavyohitajika kisheria.

“Agizo hili, sifa zake kifedha na awamu za utekelezaji, hazikutimiza mahitaji na matarajio ya muungano,” alisema.

Alilaumu Tume kwa kujaribu kuhujumu mkataba uliopo na kukiuka wajibu wake.

Kufuatia changamoto za kifedha zinazochipuka na hatua ya serikali kupunguza bajeti, SRC ilitangaza wiki iliyopita hatua ya kuwasimamishia mishahara watumishi wote wa umma kwenye bajeti ya 2024-2025.

“Taasisi za utumishi wa umma zenye CBA iliyoathiriwa na hatua ya kuahirisha utekelezaji wa nyongeza ya mishahara katika bajeti ya 2024-2025 zimeshauriwa kushirikisha miungano yao ya wafanyakazi mtawalia,” ilieleza kupitia barua iliyoandikwa Julai 18, 2024.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Lynn Mengich, alisema wataendelea kuangazia hali na kujadili marekebisho kutegemea iwapo fedha zitapatikana jinsi watakavyoshauriwa na Hazina Kuu.

Bi Mengich alisema uamuzi huo umefanyika kufuatia mashauriano ya kina na Hazina Kuu na kwa kuzingatia kanuni zilizoorodheshwa kwenye Kifungu 230(5) cha Katiba, ili kuhakikisha ustawishaji wa mswada kuhusu malipo ya umma.

Akirejelea hatua ya kufutiliwa mbali kwa Mswada wa Fedha 2024, Bw Asingo alikosoa SRC kwa kuambatisha utekelezaji wa mkataba baina yao kwenye miswada inayotarajiwa na isiyojulikana.

“SRC haipaswi kuruhusiwa kubadilisha mikataba katikati, kuahirisha au kushinikiza miungano ya sekta za utumishi wa umma kujadili upya.”