Habari Mseto

Watoto wafunzwa kujua haki zao mapema ili kupaza sauti kuhusu maovu

Na SAMMY KIMATU July 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KUNA umuhimu wa watoto kuwezeshwa kufahamu juu ya haki zao ndiposa wapaze sauti zao na kuwa na usemi katika jamii wanapoendelea kukua na kuwa watu wazima.

Mtaalamu na Mshauri katika Shirika la TIFAH, Bi Sarah Florence alisema kuna kukithiri kwa visa vya watoto kudhulumiwa wakitumika kusafirisha mihadarati, vileo haramu na pia kudhulumiwa kingono hasa katika mitaa ya mabanda Kaunti ya Nairobi.

“Watu wabaya huwaharibu watoto wetu kwa kuharibu fikra zao wanapowatuma vibandani na madukani kuwanunulia miraa, muguka, sigara na pombe miongoni mwa bidhaa nyingine,” Bi Florence asema.

Mtaalamu wa ushauri Bi Sarah Florence akizungumza na watoto wa River Bank PEFA South B Academy, kaunti ndogo ya Makadara. Picha|Sammy Kimatu

Alisema hayo katika mkutano na wanafunzi katika River Bank PEFA South B Academy kaunti ndogo ya Makadara, Ijumaa.

Aliomba mahakama kushughulikia kesi za dhuluma juu ya watoto kuharakishwa ndiposa haki ipatikane kwa watoto walioathiriwa.

Kuhusu maandamano yaliofanywa na Gen Z, alisema maandamano hayo japo yamo kikatiba, wanafunzi ndio walioathirika pakubwa kwa kukosa masomo siku mbili kwa kila wiki kukiwa na maandamano.

Aliongeza kwamba usalama wa watoto huwa katika hali ya hatihati wakati kuna maandamano na kutaka wazazi kuhakikisha watoto wako mahali salama wakati wako nyumbani.

Mwalimu katika shule hiyo, Bw Brian Otim aliambia Taifa Leo kwamba wanafunzi wake wamepigwa jeki kupitia kwa vikao na mshauri huyo ili kukumbatia mafunzo yanayowaongoza kuwa na maadili mema na kujiepusha kwa ndoa za mapema na kujitenga mbali na uhusiano wa mihadarati.

“Nimeona kuna faida kubwa kwa wanafunzi wetu tangu waanze kupata mafunzo haya. Watoto wetu ni nambari moja kwa upande wa nidhamu na pia ni wazuri katika mitihani darasani,” mwalimu Brian asema.

[email protected]