• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
Bora kitabu, wazazi wanunulia wanao vitabu kuukuu barabarani

Bora kitabu, wazazi wanunulia wanao vitabu kuukuu barabarani

NA RICHARD MAOSI

Maduka yanayouza vitabu katika miji mingi nchini yamevuna pakubwa muhula huu wa kwanza wanafunzi wanaporejea shuleni rasmi baada ya likizo ndefu.

Harakati za hapa na pale zikionekana zaidi kuwaponza wazazi waliosubiri hadi dakika ya mwisho ili kufika madukani.

Wauzaji katika maduka ya kijumla katikati ya miji na wale wa rejareja kandokando ya barabara wakionekana kupata faida kupita kiasi wakati huu ambapo biashara ya vitabu imepata mashiko na kunoga kila sehemu.

Tangu tarehe 2 Januari mwaka huu maduka ya kununua vitabu na sare yalifurika wanafunzi wenye ari ya kukata kiu masomoni kupitia elimu.

Wakiandamana na wazazi wao wameonekana wakipiga foleni ndefu, na kuwalazimu wafanyibiashara kuwahudumia kwa zamu ili kudhibiti msongamano unaozidi kushuhudiwa kila siku kiwango cha kuhofisha.

Wengine wameamua kuvinunua barabarani badala ya maduka yaliyoidhinishwa na serikali wakihofia mfumuko wa bei ghali.

Kwao bora kiwe ni kile kitabu kinachohitajika shuleni bila kujali yaliyomo.

Baadhi ya wazazi waliofurika katika maduka ya kuuza vitabu katika Kaunti ya Nakuru kwenye barabara ya Kenyatta. Picha/Richard Maosi

Kulingana na wachapishaji vitabu bei ghali inatokana na ushuru wa hadi asilimia 16.Kinyume na mataifa mengine duniani ambapo sekta ya elimu haitekelezi ushuru kwenye vitabu.

Mwandishi Jeff Mandila anasema kizazi cha kesho kinategemea yaliyonakiliwa ndani ya vitabu.”Vijana wahamasishwe kwenye makongamano kuvalia njuga swala la kusoma vitabu sahihi kwani masomo ni ghali ,”alisema.

Mwaka uliopita baadhi ya madai yaliyochipuka kutoka kwa wakuu wa shule yalidhibitisha kuwa vitabu vilikuwa vikiibiwa kutoka shuleni na hatimaye kuuzwa sokoni.

“Wauzaji wengine wamekuwa wakiuza vitabu hata katika nchi jirani ya Uganda na Tanzania,”alieleza mwalimu Peter Songok kutoka Lanet.

Tulitaka kujua mbona wanunuzi wengi hupendelea kununua kutoka kwa wauzaji rejareja licha ya ukosefu wa ubora unaostahili na marufuku ya serikali miaka ya nyuma, na haya hapa ndio baadhi ya maoni yao.

“Vitabu kuu kuu vinatupunguzia gharama ya masomo humu nchini inayozidi kuwa kubwa kila mwaka.Ni kama serikali imewatwika wazazi mzigo mzito wa kujielimishia watoto”Bi Betty Maina alisema.

Akiwa ni mzazi anayepania mwanawe wa kiume ajiunge na shule ya upili ya Menengai .

Kwa mfano Biblia ya Good News katika duka la kijumla inauzwa 802,huku wauzaji wa wa rejareja wakitoza kati ya 500-600.

Ushindani mkali ulikuwa ni kati ya wauzaji kwenye maduka makuu na wale wenye mtaji kidogo wanaojitegemea kuuza vitabu kuu kuu barabarani. Picha/ Richard Maosi

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali muuzaji Wycliffe Ombaka ambaye amekuwa akifanya biashara hii kwa zaidi ya mwongo mmoja anasema hajawahi kushuhudia wanunuzi wengi kama mwaka huu 2019.

Anasema vilevile wazazi wengi hawana imani na vitabu vinavyosambazwa na serikali ndio sababu wakaamua kujitafutia mbinu ya kuwaelimisha watoto wao.

“Mwaka uliopita serikali ilinyoshewa kidole cha lawama kwa makosa yaliyojaa ndani ya vitabu vya shule ya msingi na upili,”Ombaka alisema.

Licha ya kugharamia vitabu hivyo hatimaye havijawafaidisha wanafunzi na kufanya sekta ya elimu izidi kudorora.

Mwaka wa 2019 KICD ilitoa utaratibu wa kukagua vitabu halali na vile haramu kwa kuzingatia mambo yafuatayo.

Kwanza kutuma nambari ya siri kwa 22776 ili kutambua endapo kitabu kulichonunuliwa kilikuwa kimeidhinishwa na taasisi ya elimu KICD.

Pili nembo ya KICD kuwa kwenye majalada ya vitabu ili kubaini ubora wake kabla ya kutumika na wanafunzi.

You can share this post!

Droo ya timu za Afrika Mashariki kuchuana na Everton yatajwa

Mwandishi akaangwa kudai wanawake wazee hawawezi kumsisimua...

adminleo