ODM yaonya wanachama wake wanaomezea mate uwaziri
CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) cha Raila Odinga kimeonya wanachama wake wanaomezea mate nyadhifa serikalini kikisema hakitaki kujiunga na serikali ya Rais William Ruto.
Chama hicho mnamo Jumanne kilionya wanachama wake dhidi ya kuteuliwa katika Baraza la Mawaziri, tangazo ambalo limeongeza mkanganyiko katika mipango ya ODM ya kujiunga na serikali Muungano wa Kitaifa inayopendekezwa.
Katika taarifa, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alifichua kuwa baadhi ya wanachama wao tayari walikuwa wakimezea mate nyadhifa za uwaziri na nyingine serikalini.
“Kumekuwa na dhana kwamba ODM inatamani sana kujiunga na serikali ilhali muda wote tumekuwa wazi kwamba tunachotaka ni mazungumzo ya kitaifa ambayo yanapaswa kutanguliwa na kuwepo kwa mazingira muhimu kupitia utekelezaji wa masharti ambayo tumetoa kama chama,” Bw Sifuna alisema katika taarifa.
“Mwanachama yeyote wa ODM anayejitolea kujiunga na baraza la mawaziri la Kenya Kwanza au wadhifa wowote mwingine anapaswa kujua kwamba anafanya hivyo bila baraka au uungwaji mkono wa chama,” Bw Sifuna alionya.
Bw Sifuna alisema chama hicho hakikuwa katika mazungumzo yoyote na utawala wa Rais Ruto kuhusu muungano au mpangilio wowote wa kisiasa.
ODM ya Bw Odinga iliripotiwa kutengewa nafasi tatu katika Baraza la Mawaziri Rais Ruto alipotaja kundi la kwanza la mawaziri wateule 11. Mpango wa awali ulikuwa ni kwa Rais kutaja nafasi 14. Majina hayo matatu yaliripotiwa kufutwa baada ya Bw Odinga kumtaka Dkt Ruto kushughulikia baadhi ya matakwa ya vijana ambao wamekuwa wakiandamana.
Katika taarifa hiyo, chama hicho kilidumisha ‘msimamo wake usioyumbayumba wa kuunga mkono mapambano yanayoendelea ya kutafuta suluhu ya kudumu ya muda mrefu ya masuala ya utawala yanayoibuliwa na Gen Z.’
Chama hicho kilikariri njia ya kutatua mzozo wa sasa wa kisiasa ni kupitia mazungumzo ya kitaifa kwa uaminifu na yanayopaswa kujumuisha Wakenya wote.
“Chama cha ODM kinaendelea kushikilia msimamo wake na mapambano yanayoendelea ya kutaka Kenya bora. Tutaendelea kusimama na wananchi na kupigania haki na kuleta marekebisho ambayo taifa letu linahitaji sana,” chama hicho kilisema.
Mnamo Jumapili, Bw Odinga alisisitiza kuwa haki lazima itangulie mazungumzo yoyote. Alitoa masharti kadhaa ambayo lazima yatimizwe kabla ya mazungumzo ya kitaifa kufanyika.
Haya ni pamoja na fidia kwa waathiriwa wa ukatili wa polisi, kuondolewa kwa kesi zote zinazohusiana na maandamano na kuachiliwa kwa wale wote waliotekwa nyara na kuzuiliwa wakati wa maandamano.
Bw Odinga pia ametaka kusuluhishwa kwa masuala yanayohusu afya na elimu hasa kuajiriwa kwa walimu wa shule za sekondari msingi.
Alisema ni lazima Rais Ruto arejeshe Mpango wa Kitaifa wa Bima ya Afya wa NHIF na kufutilia mbali SHIF.
Pia anataka maafisa wa sekta ya usalama wafunguliwe mashtaka kwa kuhusika na ukatili dhidi ya waandamanaji waliodumisha amani.
Bw Odinga alipendekeza masuala haya yakitatuliwa, mazungumzo ya kitaifa yanaweza kufanywa katika ukumbi usioegemea upande wowote na wawakilishi kutoka sekta mbalimbali, wakiwemo vijana, serikali, viongozi wa kidini, wataalamu wa afya, mawakili na walimu.
Anapendekeza kuwa mkutano mkuu wa kitaifa ushughulikie masuala muhimu ya kitaifa na kikatiba kama vile utawala bora, kupanda kwa gharama za maisha, kuangamiza ukabila, vita dhidi ya ufisadi na usimamizi wa madeni na sera ya fedha.