Habari za Kitaifa

Raila sasa ajitenga na uteuzi wa mawaziri 4 wa chama chake ODM

Na MOSES NYAMORI July 26th, 2024 2 min read

KIONGOZI wa Upinzani Raila Odinga jana alikanusha kuwa ana mkataba wa kisiasa na UDA inayoongozwa na Rais William Ruto licha ya maafisa wake wanne kuteuliwa mawaziri mnamo Jumatano.

Katika hatua iliyoonekana kujaribu kuepuka hasira za vijana wanaomlaumu kwa hatua ya kukubali kuungana na serikali wanayopinga, Bw Odinga alisema chama na Azimio hazikuamua kushirikiana na Kenya Kwanza.

Bw Odinga kupitia taarifa jana alisema wanne hao John Mbadi, Hassan Joho, Opiyo Wandayi na Wycliffe Oparanya, wamejiunga na utawala wa Kenya Kwanza kama watu binafsi.

Hata hivyo, hakubainisha iwapo aliwapa baraka zake huku akiwatakia kila la kheri na kuwataka watumie vyeo hivyo kubadilisha nchi.

“Jinsi ilivyoandikwa kwenye taarifa yetu mnamo Julai 23, 2024 ODM au Azimio la Umoja hazijaungana na utawala wa Rais William Ruto,” akasema Bw Odinga.

Aliongeza kuwa, ODM ilikuwa inatarajia kushirikiana tu na serikali baada ya kuundwa kwa mwongozo wa kuyatatua masuala ambayo yaliibuliwa na Gen Z.

Kati ya masuala hayo ni fidia kwa familia ambazo watu wao waliuawa baada ya kutekwa, wale waliojeruhiwa wakati wa maandamano ya upinzani mwaka jana na kushtakiwa kwa polisi ambao waliwaua waandamanaji.

“Japo tunawatakia walioteuliwa kila la heri na kuonyesha imani watachangia kujenga taifa hili, bado tunapigia debe mazungumzo kwa msingi wa masharti ambayo tuliyatoa,” akasema.

Kauli hii ilionekana kurejelea matakwa ya vijana na vinara wenza wa Azimio ambao wamekataa kujiunga na serikali.

Bw Odinga alisema chama chake kinasalia imara katika kudumisha msingi wa demokrasia, uongozi bora na haki ya kijamii.

Hata hivyo, hatua ya ODM kusisitiza kuwa haijajiunga na UDA inaonekana kama mbinu ya kuhakikisha inasalia na viti viwili vya hadhi katika uongozi wa bunge.

Iwapo ODM ingekubali kuwa imeanza ushirikiano wa kisiasa na Kenya Kwanza, basi vyama tanzu ndani ya Azimio hasa Wiper na Jubilee ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, vingeendea nyadhifa za Kiongozi wa Wachache na Uenyekiti wa Kamati ya Uhasibu Bungeni (PAC).

Nyadhifa hizo mbili zilikuwa zikishikiliwa na Wandayi na Bw Mbadi ambao hawatakuwa na jingine ila kujiuzulu iwapo uteuzi wao wa kuunga baraza la mawaziri utaidhinishwa na Bunge la Kitaifa.

Kisheria, ODM ndiyo inastahili kushikilia nyadhifa hizo kwa kuwa ndicho chama kilichoshinda viti vingi baada ya UDA anayoiongoza Rais Ruto.

Mnamo Jumatano, Rais Ruto aliwateua Bw Mbadi ambaye pia ni mwenyekiti wa ODM kama Waziri wa Fedha, Bw Wandayi (Kawi na Mafuta), Gavana wa zamani wa Kakamega Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika) na Gavana wa zamani wa Mombasa Hassan Joho (Madini na Uchumi Baharini).

Bw Joho na Bw Oparanya wote ni manaibu viongozi wa ODM naye Bw Mbadi ni mwenyekiti huku Bw Wandayi akiwa kiongozi wa masuala ya kisiasa na kiongozi wa wachache bungeni.

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna mnamo Jumatano asubuhi alisisitiza kuwa wanne hao walijiunga na utawala wa Kenya Kwanza kama watu binafsi.

“Je tuliwajua watu ambao tulikuwa tunazungumza nao, ndio. Ni jambo ambalo lilifuata sheria za chama, la. Tuliidhinisha hatua ya wanne hao kujiunga na serikali, hapana. Kwa hivyo, huu si uamuzi wa ODM,” akasema Bw Sifuna.

“Natarajia kuwa kabla hawajaenda kuhojiwa na Bunge, watatuma barua za kujiondoa kwenye nyadhifa wanazoshikilia. Matarajio yangu ni hayo kwa sababu hawawezi kujiunga na baraza la mawaziri kama wanachama wa ODM na pia bado wana vyeo ndani ya chama,” akaongeza Bw Sifuna.

Hata hivyo, Seneta wa Kisumu Tom Ojienda amesema ni jambo lisilowezekana kwa wanasiasa hao wanne kujiunga na mrengo wa Dkt Ruto bila idhini ya Bw Odinga.

“Mbadi, Joho, Oparanya na Wandayi hawawezi kuteuliwa kwenye baraza la mawaziri na Rais Ruto bila baraka za Raila. Watahitajika wajiuzulu kwenye nyadhifa zao ndani ya bunge na kwa chama cha ODM,” akasema Bw Ojienda.