Habari za Kitaifa

ODM yaanika ulafi wa kisiasa ikikwamilia viti vya upinzani bungeni

Na BENSON MATHEKA July 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

TABIA ya ubinafsi na tamaa ya chama cha ODM ya kutaka kutawala vyama tanzu katika miungano ya kisiasa imechipuka tena ikitaka kukwamilia nyadhifa za uongozi katika upinzani bungeni hata baada ya kuwa wazi imejiunga na serikali.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga amejaribu kukanusha kwamba chama chake kimejiunga na Serikali katika kile ambacho wachanganuzi wanasema ni uroho wa kutaka kukwamilia nyadhifa za uongozi bungeni.

Kulingana na Raila, viongozi wa chama chake walioteuliwa mawaziri walifanya hivyo kama watu binafsi na haukuwa uamuzi wa ODM au muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

Kauli sawa ilitolewa na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna aliyedai kuwa hakukuwa na azimio la chama, viongozi  wake wateuliwe mawaziri.

Baada ya Rais William Ruto kuwateua maafisa wanne wa ODM kuwa mawaziri, vinara wenza wa Azimio walimtangaza kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kuwa kiongozi mpya wa muungano wa upinzani.

Hata hivyo, kundi la wanachama wa ODM eneo la Nyanza liliwashutumu kwa kujaribu kumpindua Raila kutoka wadhifa wake wa sasa katika  muungano huo wa upinzani.

Wadadisi wanasema  hatua ya Raila na ODM ni kutaka kuthibiti  upinzani akiwa serikalini. “ Ni tamaa ambayo alionyesha mara ya kwanza baada ya handisheki yake na Uhuru Kenyatta 2018 japo wakati huo wandani wake hawakuteuliwa mawaziri,” asema mchambuzi wa siasa Collins Mwenda.

Anasema lengo la Raila na ODM ni kukwamilia nyadhifa za kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa na seneti na viranja wa wachache katika mabunge hayo ambazo zinashikiliwa na ODM kama chama kikubwa katika Azimio.

“Hii ndiyo sababu inafanya washirika wa Raila kupiga kelele wakilaumu Kalonzo na wenzake waliokataa kujiunga na serikali kwa kumpindua kiongozi wao kama kinara wa Azimio,” asema.

Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi aliyeteuliwa waziri wa kawi na petroli ndiye kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa huku mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed, mwandani wa karibu wa Raila akiwa kiranja wa wachache.

Nyadhifa hizi na zile za seneti huwa za kifahari kwa kuwa afisi zinafadhiliwa na Tume ya Huduma ya Bunge na wanaozishikilia wanapata marupurupu mengi yakiwemo magari ya serikali.

Mnamo Alhamisi,  Musyoka alitangazwa na wenzake kuongoza muungano huo huku Bw Odinga akijikita kwenye “kampeni za kuwania uenyekiti wa Tume ya  Afrika”.

Kulingana na gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, ODM hatua ya Musyoka na vinara wenza wa Azimio ni ya kumtimua Raila katika muungano huo.

“Sisi ni wanachama thabiti wa muungano wa Azimio na siku ambayo Raila Odinga ataondoka kwenye kiti atasema. Ni kana kwamba amepinduliwa kutoka kwa uongozi kwa kisingizio kwamba anaenda AU,” alisema Wanga.

Mwenda anasema hatua ya ODM ya kukwamilia uongozi wa Azimio bungeni ni kilele cha uroho, tamaa na unafiki wa kisiasa.

“Nashawishika kuwa kauli ya Sifuna kwamba kuteuliwa kwa wenzake katika baraza la mawaziri hakukuwa uamuzi wa chama kama njia ya kukwamilia wadhifa wake kama naibu kiongozi wa wachache katika seneti. Hii ni kwa sababu wenzake, baadhi yao walio karibu sana na Raila kama Peter Kaluma na Mbadi mwenyewe walikiri kwamba chama kiliamua wajiunge na serikali,” akasema.

Anasema Raila amejiweka katika hatari ya kuamuliwa mustakabali wake wa kisiasa na Rais Ruto.