Habari za Kitaifa

Tumetenga, tutafanya, Ruto aendelea kumimina ahadi

Na LUCY MKANYIKA July 28th, 2024 2 min read

RAIS  William Ruto Jumapili aliendelea kutoa ahadi chungu nzima kwa Wakenya huku akisema utawala wake utapunguza utekelezaji wa miradi kutokana na hatua aliyochukua ya kuondoa Mswada wa Fedha 2024/25.

Rais Ruto alisema alilenga kupata pesa zaidi kupitia ushuru ambao ulikuwa umependekezwa kwenye mswada huo uliopingwa vikali na Wakenya na kuchangia maandamano nchini.

“Kwenye bajeti ya mwaka huu wa kifedha nilikuwa nimepanga kutekeleza mengi lakini kulikuwa pia na propaganda nyingi. Sasa lazima nitafute njia nyingine lakini ni vyema kutotilia manani propaganda na habari feki,” akasema Rais Ruto.

Alikuwa akiongea katika Kaunti ya Taita Taveta wakati wa ibada kwenye Kanisa la Kianglikana ya St Peters Bura, Kaunti ndogo ya Mwatate.

Aliwataka Wakenya wavumilie serikali yake kwa sababu sasa hawawezi kuzindua miradi mipya kutokana na upungufu wa fedha uliopo kwenye bajeti.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya kusema hayo, Rais aliendelea kutoa ahadi tele kwa wakazi wa kaunti hiyo akisema atazuru eneo hilo kuzindua miradi mipya kaunti ndogo za Mwatate, Taveta na Voi.

Japo wakazi walikuwa wakisubiri kufahamu hatua zilizopigwa katika kutekeleza miradi iliyozinduliwa hapo awali, Rais alikwepa suala hilo kabisa.

Baadhi ya miradi aliyozindua na haijaanza ni mradi wa mabomba ya maji wa Mzima Two, Barabara ya Taveta-Illasit na ile ya Bura-Mgange-Mbale –Mtomwagodi.

“Nilikuwa nimetenga pesa kwa barabara ya Bura-Mghange-Mbale-Mtomwagodi lakini mnajua kile kilichotokea,” akasema kabla kuzungumzia masuala mengine.

Mradi wa ujenzi wa makazi ya gharama nafuu ndio unatarajiwa utazinduliwa na Rais Mwatate, Taveta na Voi akizuru tena kaunti hiyo jinsi alivyoahidi.

Alisema nyumba 800 zitajengwa Mwatate na nyingine 1,000 Voi na Taveta.

Rais alisema serikali itashirikiana na mwekezaji ambaye amekubali kuanzisha kiwanda cha chuma kwa kima cha Sh10 bilioni Voi. Kulingana naye, kiwanda hicho kitawapa zaidi ya vijana 2,000 ajira.

Aliongeza kuwa serikali imetenga Sh500 milioni kuunganisha umeme kwenye nyumba 10,000 katika kaunti hiyo na pia itawajengea nyumba za wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Taita Taveta na kile cha kiufundi cha Taita Taveta.

Aliendelea kuahidi akisema ataketi chini na uongozi wa kaunti hiyo kuweka mipango jinsi ambavyo miradi ya maendeleo itaendelea kutekelezwa katika kaunti hiyo.

Wakati wa hafla hiyo, kiongozi wa nchi alitetea uamuzi wake wa kuwaingiza viongozi wa upinzani serikalini, akisema hilo litasaidia kuhakikisha kuna umoja na taifa linasonga mbele hasa baada ya maandamano ya Gen Z.

“Kile kilichofanyika kimetuwezesha kuanzisha mwelekeo mpya nchini. Baraza jipya la mawaziri litatuunganisha na sasa tumeweka siasa za vyama kando na kuipa umoja wa nchi mstari wa mbele,” akasema.

Gavana Andrew Mwadime, wabunge John Bwire (Taveta), Peter Shake (Mwatate) na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa kaunti hiyo Lydia Haika waliahidi kushirikiana na serikali kuhakikisha miradi iliyokwama inakamilika na mingine mipya inaanzishwa.

“Tumekuwa kwenye kijibaridi kwa miaka mingi na sasa tuna matumaini kuwa miradi mingi itatekelezwa na watu wetu wanufaike,” akasema Bw Shake.