Habari za Kitaifa

Polisi wa Kenya wakomboa mji wa Gauthier, Haiti baada ya mapigano makali


POLISI wa Kenya ambao wapo nchini Haiti kupiga jeki juhudi za kuleta udhabiti Jumamosi walikabiliana na magenge katika kisa kilichogubikwa na ufyatulianaji mkali wa risasi mjini Gauthier.

Kamanda wa kikosi cha Kenya Godfrey Otunge alisema polisi walikabiliana na magenge hayo kwa saa kadhaa na kutwaa mji huo ambao umekuwa himaya ya magenge hatari kwa serikali.

“Halikuwa jambo rahisi kwa sababu polisi walikabiliana sana na magenge hayo na kuchukua usimamizi wa mji huo. Hata sasa wanasimamia kituo cha polisi cha Gatheri,” akasema Bw Otunge.

Picha ambazo Taifa Leo iliziona ilionyesha jinsi ukuta wa kituo hicho cha polisi uliangushwa na sehemu yake kuchomwa. Mji wa Gatheri umekuwa chini ya usimamizi wa genge la wanachama zaidi ya 400 ambalo linafahamika kama Mawazo.

Wanachama wa genge hilo waliwatupia polisi kutoka Kenya mabomu ya petroli kwa lengo la kuwatia hofu. Gari ambalo polisi walikuwa wakitumia wakati wa shambulio hilo lilipasuliwa dirishani.

Hii ilikuwa mara ya pili ambapo polisi Wakenya walilazimika kutumia risasi dhidi ya magenge. Mara ya kwanza ilikuwa mnamo Julai 17, 2024 wakati ambapo walitwa bandari ya Autorite Portuaire Nationale (APN).

Mnamo Jumamosi wikendi iliyopita, Balozi wa Canada kule Haiti Andre Francois Giroux alikutana na Bw Otunge na kuzungumzia operesheni hiyo.

Bw Giroux aliteuliwa mnamo Novemba 2023 na alisema kuwa Canada inapanga kuwatuma maafisa wake wa usalama kusaidia kurejesha udhabiti Haiti.