Habari za Kaunti

Wakazi wataka CCTV kuzima wizi Mpeketoni

Na KALUME KAZUNGU July 29th, 2024 2 min read

WAKAZI wa mji wa Mpeketoni, Kaunti ya Lamu wameishinikiza serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kuweka kamera za CCTV kwenye mitaa na vichochoro vya mji huo kusaidia kukabiliana na wizi na uhalifu mwingine.

Mpeketoni ni mji unaotambulika kuwa wa kibiashara na ukulima kote Lamu.

Siku za hivi karibuni, kumeshuhudiwa visa vya wizi hasa kuvunjwa kiholela kwa maduka ya kielektroniki na vyombo kuibwa.

Katika mahojiano na Taifa Leo Jumapili, wakazi, wengi wao wakiwa ni wanabiashara walisema kuwekwa kwa CCTV mjini humo kutasaidia pakubwa kukabiliana na wezi na hata kuwatambua.

Bw John Musyoka alisema hairidhishi kuona wezi wakitekeleza maovu yao na kutoweka bila kutambuliwa na kuchukuliwa hatua.

“Mbali na kuimarisha usalama, tunaamini kamera za CCTV zitasaidia kuwatambua wakora hao, wakamatwe na wachukuliwe hatua kali za kisheria. Kaunti, serikali kuu na wahisani wajikaze kutuwekea hizo CCTV hapa. Tumechoka kuvunjiwa maduka na vifaa kuibwa,” akasema Bw Musyoka.

Lucy Ng’ang’a, mwanabiashara mjini Mpeketoni, alipendekeza endapo kamera hizo zitawekwa basi zihudumu kwa masaa yote.

Alisema kuwepo kwa CCTV kutasaidia kuwafurusha wakora mjini wakifahamu fika kuwa huenda wakajipata sura zao zikinaswa, hivyo kutambulika.

“Kamera ziwekwe. Kwa sasa wanavunja na kuiba madukani wakiwa na ujasiri wote wakijua fika kuwa hakuna anayewamulika,” akasema Bi Ng’ang’a.

Wakazi hata hivyo waliomba idara ya usalama pia kuongeza doria usiku na mchana mjini Mpeketoni na viunga vyake ili kukabiliana na uhalifu wa aina yoyote ile.

“Kukiwa na doria za kila mara, iwe ni za polisi au jeshi, wakora wanaoendeleza maovu yao wataogopa na kuhama huu mji wetu,” akasema Bw Simon Mbuthia.

Mwezi uliopita, washukiwa wanne wa wizi na ufunguaji wa simu za M-Kopa walinaswa kwenye msako mkali uliotekelezwa ghafla na polisi mjini Mpeketoni.

Wanne hao, ikiwemo wanaume watatu na mwanamke mmoja, walinyakwa kwenye maduka tofauti tofauti mjini humo, ambapo jumla ya simu 76, ikiwemo za kawaida na zile za M-Kopa, vipakatalishi na vifaa vingine vinavyowasaidia kutekelezea ujanja na wizi huo vikinaswa.