Habari za Kitaifa

Malala akabiliwa na upinzani UDA


SARAKASI zilishuhudiwa katika makao makuu ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) Jumanne, Julai 30, 2024 baada ya baadhi ya wanachama kudai kumwondoa afisini Katibu Mkuu,  Cleophas Malala.

Wakiongozwa na wakili Joe Khalende, kundi hilo linalojiita  “Waanzilishi wa UDA” walimsuta Malala wakidai anadumaza maendeleo ya chama hicho na serikali ya muungano iliyoundwa na kiongozi wa chama,  Rais William Ruto na kiongozi wa ODM,  Raila Odinga.

Khalende na wenzake pia walimshutumu Bw Malala kwa kushirikiana na viongozi wa Vuguvugu la TAWE linaloongozwa na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya, kinyume cha katiba na maongozi ya UDA.

Akiongea na wanahabari, wakili huyo alijitangaza kuwa kaimu mpya wa Katibu Mkuu wa UDA na kwamba Malala amezimwa kuendesha majukumu yote ya afisi hiyo.

“Malala ametelekeza wajibu  na majukumu yake kama Katibu Mkuu wa chama chetu cha UDA. Miongoni mwa majukumu hayo ni kuwa msemaji wa chama na kuitisha mikutano yote. Sasa hafanyi hayo na badala yake ameungana na wapinzani wetu. Anaunga mkono vuguvugu la TAWE na ajenda ambazo zinakinzana kabisa na za chama chetu ambacho ndicho chama tawala nchini,” Bw Khalende akasema.

“Ameenda kinyume na matakwa ya kiongozi wa chama chetu. Anapinga kuundwa kwa serikali mpya ya muungano na niko hapa kuthibitisha kuwa yeye sio Katibu Mkuu wa UDA tena na ndimi Joe Khalende ndiye nitaanza kuhudumu kama Katibu Mkuu wa chama chetu,” akasema.

Bw Khaende hata hivyo alikataa kujibu swali kuhusu iwapo kiongozi wa chama Rais Ruto au asasi yoyote ya UDA imeidhinisha mapinduzi hayo.

“Maswali yenu yatajibiwa hivi karibuni Baraza Kuu la Kitaifa la UDA litakapokutana. Lakini kabla ya kufanyika kwa mkutano huo, mimi ndiye nitakuwa nikiendesha majukumu yote ya Katibu Mkuu wa UDA,” akasema.

Lakini dakika chache baada ya Bw Khalende kujitangaza kuwa Katibu Mkuu mpya wa UDA,  Bw Malala alipuuzilia mbali madai yake kama ‘propaganda’ zisizo na msingi wowote.

“Puuzeni hizo propaganda. Chama kiko imara na kinaendelea kumsaidia Rais William Ruto kutekeleza ajenda yake kwa Wakenya. Chama kiko imara!” Bw Malala akasema kupitia mtandao wa X (zamani Twitter).