Kimataifa

Harris mbele ya Trump katika majimbo makuu kulingana na kura za maoni

Na MASHIRIKA July 31st, 2024 1 min read

WASHINGTON, AMERIKA

UMAARUFU wa mgombeaji urais wa chama cha Democratic, Kamala Harris unaendelea kupanda huku kura za maoni zikionyesha kuwa anaongoza katika majimbo makubwa.

Harris yuko mbele ya Trump katika majimbo manne muhimu wakati rais huyo wa zamani akiwa mbele katika mawili, kulingana na kura ya maoni ya Bloomberg News/Morning Consult.

Harris anaongoza katika jimbo la Michigan kwa asilimia 11, pia anaongoza Arizona, Wisconsin na Nevada, kulingana na kura ya maoni.

Naye Trump ana umaarufu North Carolina.

Ikiwa uchaguzi ungefanyika leo, basi anayeongoza katika jimbo la Georgia angeshinda.

Katika kura ya maoni iliyoidhinishwa na Taasisi ya Maendeleo ya Kidemokrasia ( PAC), Harris anaongoza kwa asilimia kubwa katika jimbo la Georgia, huku Trump akiwa mbele kwa alama mbili majimboni Arizona na Pennsylvania.

Katika kura ya maoni iliyofanywa kote nchini na Reuters/Ipsos, Harris anaongoza kwa asilimia 43.

Harris, ambaye atatajwa rasmi kupeperusha bendera ya chama cha Democratic hapo Jumatatu, anatarajiwa kutangaza mgombea mwenza wake ndani ya siku chache kabla ya kuanza ziara ya majimbo ambayo yataamua uchaguzi wa Novemba 5.

Gavana wa Pennsylvania, Josh Shapiro, Seneta wa Arizona, Mark Kelly na Waziri wa Uchukuzi, Pete Buttigieg, miongoni mwa wengine, wametangaza azma ya kuwa mgombea-mwenza wa Harris.

Tangu Rais wa nchi hiyo, Joe Biden kujiondoa katika uchaguzi ujao wa Novemba 5, 2024 na kumpendekeza makamu wake kupeperusha bendera ya chama chao, Harris, amepata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi mbalimbali.

Siku mbili zilizopita, Harris alikuwa amechangiwa Sh26 bilioni za kufanya kampeni. Isitoshe, zaidi ya wahisani 170,000 wamejitolea bila malipo kumsaidia Harris katika shughuli za kumpigia debe.