Wakenya sasa kutumia bajeti ya serikali ya Kenyatta baada ile ya Ruto 2023 kuzimwa kortini
SERIKALI ya Rais William Ruto imepata pigo kuu la kihistoria baada ya mahakama ya rufaa kuharamisha Sheria ya Fedha ya 2023.
Sasa Ruto atatumia Sheria ya Fedha ya Serikali ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kukusanya ushuru wa kufadhili huduma za serikali ya Kenya Kwanza.
Kufuatia kuharamishwa kwa sheria hii ya Fedha ya 2023, sheria ya makato ya nyumba (housing levy) ni haramu kwa vile yanatokana na sheria hii iliyopigwa kalamu.
Majaji Kathurima M’Minoti, Agnes Murgor na John Mativo waliharamisha sheria hii ya Fedha ya 2023 wakisema inakinzana na Katiba.
Uamuzi huu wa majaji hawa umeletea afueni Wakenya waliokandamizwa na kuongezwa kwa ushuru wa mafuta kutoka asilimi mia nane (8) hadi kumi sita (16).
Majaji hawa wa mahakama ya pili kwa ukuu nchini walisema utaratibu uliopelekea kupitishwa kwa Sheria ya Fedha 2023 ulikaidi Katiba, umepotoka na hauna mashiko kisheria.
“Baada ya kutathmini mawasilisho ya Seneta Okiya Omtatah na walalamishi wengine, tumefikia uamuzi kwamba kupitishwa na kutiwa sahihi kwa Sheria ya Fedha 2023 kulikiuka Vifungu vya Katiba 220 (1) (a) na 221 pamoja na sehemu nambari 37, 39A, na 40 vinavyotoa utaratibu na mwelekeo wa kuandaliwa kwa Sheria ya Fedha,” majaji hao walisema.
Kukaidiwa kwa utaratibu na mwongozo uliowekwa umetweza na kupotoka.
Hivyo basi majaji hao walisema Sheria ya Fedha 2023 inakiuka katiba na haina mashiko na kamwe na “imeharamishwa.”
Majaji Kathurima, Murgor na Mativo walisema kesi ya Bw Omtatah imethibitisha kwamba Sheria ya Fedha ya 2023 ni kinyume cha sheria na kamwe haipasi kutumika kuwatoza wananchi ushuru.
Sasa ni afueni kwa wananchi kwa kuwa Sheria ya Fedha ya 2024/2025 iliondolewa na Rais William Ruto kufuatia maandamano ya Gen Z na sasa ile ya 2023/2024 imeharamishwa pia.
Wananchi sasa watatozwa ushuru kulingana na sheria ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.