Iran, Hamas waapa kulipiza kisasi kufuatia kifo cha Haniyeh
IRAN imeapa kujibu shambulio la Israeli lililomwangamiza kiongozi wa kundi la wapiganaji wa Hamas, Ismail Haniyeh.
Wakati huo huo, Hamas pia imeapa kulipiza kisasi kwa mauaji ya kiongozi wao.
Haya yanajiri huku mamia ya Wapalestina wakiandamana katika mji wa Istanbul, Uturuki
wakitaka haki itendeke baada ya Israeli kumwangamiza Haniyeh.
Jeshi la Israeli, hata hivyo, halijatoa taarifa yoyote kuhusu tukio hilo.
Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu jana alisema nchi yake imetoa “pigo kali” kwa maadui zake katika siku za hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kuuawa kwa kamanda mkuu wa Hezbollah nchini Lebanon saa chache kabla ya shambulio la Tehran.
Netanyahu pia aliwaonya Waisraeli “wajiandae kwa lolote litakalotokea”, huku kukiwa na hofu kuwa mzozo huo huenda ukaenea na kuwa mbaya zaidi.
“Tuko tayari kwa hali yoyote na tutasimama kwa umoja na kuchukua hatua mwafaka kujilinda.”
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alionya dhidi ya kuongezeka kwa uhasama katika eneo hilo.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipaswa kukutana Jumatano jioni kujadili hali hiyo.
Haniyeh, ambaye kwa kawaida anaishi Qatar, amekuwa akihusika na diplomasia ya kimataifa katika kundi hilo la Palestina huku vita vilivyoanzishwa na shambulio la Hamas dhidi ya Israeli mnamo Oktoba 7 vikipamba eneo la Gaza, ambapo wanawe watatu waliuawa katika shambulio la angani lililotekelezwa na Israel.
Akishikilia wadhifa wa juu katika eneo hilo alioteuliwa mwaka 2017, Haniyeh amekuwa akihamia kati ya Uturuki na mji mkuu wa Qatar, Doha, akikwepa njia za usafiri za Ukanda wa Gaza uliozingirwa na jeshi la Israeli kumwezesha kuwa mpatanishi katika mazungumzo ya kusitisha mapigano.