Makala

Sababu za WHO kukataza Mpox kuitwa Homa ya Tumbili/Monkeypox

Na LABAAN SHABAAN August 2nd, 2024 2 min read

UGONJWA wa homa ya tumbili (Monkeypox) uligunduliwa 1958 katika maabara nchini Denmark miongoni mwa koloni za tumbili zilizokuwa zinafanyiwa utafiti.

Kisha, kisa cha kwanza kuambukiza binadamu kilishuhudiwa kwa mvulana wa miezi 9 nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) 1970.

Nyakati hizo hakukuwa na tashwishi kuhusu matumizi ya jina la ugonjwa huo kuwa Monkeypox.

Lakini, Shirika la Afya Duniani (WHO), lilisikitishwa na visa vya matamshi ya ubaguzi wa rangi na unyanyapaa baada ya ugonjwa huo kusambaa katika zaidi ya mataifa 100.

WHO ilifichua kuwa watu na mataifa mengi yalitaka jina la monkeypox libadilishwe.

Visa 98,001 vya ugonjwa huu vimeripotiwa katika nchi 118 duniani.

Kati yao, watu 183 walioambukizwa walifariki katika mataifa 27.

Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) nchini Amerika.

Kutoka Monkeypox hadi Mpox

Ilichukua miaka 64 kwa WHO kubadili jina na kutaka dunia itumie neno Mpox kurejelea ugonjwa wa homa ya tumbili.

Mnamo Novemba 2022, shirika hili la Umoja wa Mataifa (UN) lilitangaza majina yote mawili yatumike kwa pamoja kwa kipindi cha mwaka mmoja kisha yaondolewe kabisa.

“Baada ya mfululizo wa mashauriano na wataalamu wa kimataifa, hatimaye WHO litaanza kutumia jina MPOX (kwa Kingereza) badala ya ‘Monkeypox’ au ‘homa ya Ndui ya Nyani’ kufuatia mapendekezo ya kubadilishwa kwa jina hilo kwa maelezo ya kwamba lilikuwa na athari hasi kadhaa ukiwemo unyanyapaa,” ilisema taarifa ya WHO ya Novemba 28, 2022.

Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus alipendekeza kuwa jina “Monkeypox’ halitafutwa kabisa kwenye rekodi ya Mfumo wa Kimataifa wa Uainishaji wa Magonjwa (ICD) ili kuhifadhi historia.

Ugonjwa kuwa na jina jipya ni nadra

Kubadili jina la maradhi hufanyika kwa nadra sana. Huu ni wajibu wa WHO na ICD kupitia mchakato wa mashauriano unaojumuisha nchi wanachama wa shirika hilo.

Mchakato huu hufanyika kwa miezi kadhaa hadi zaidi ya mwaka mmoja kutegemea na uzito wa ugonjwa, upatikanaji wa ushahidi wa kisayansi na athari ya ugonjwa duniani.

Lakini kwa Monkeypox, mchakato ulifanywa upesi kwa sababu kulikuwa na haja ya kukabili ubaguzi na kufuata kanuni bora za uainishaji.

Kisa cha kwanza Kenya

Mnamo Julai 31, 2024, Kenya ilithibitisha kisa cha kwanza cha Mpox katika mpaka wa Taveta na Tanzania.

Kisa cha kwanza cha Mpox katika mpaka wa Taveta na Tanzania.Picha| Maktaba

Virusi hivyo viligunduliwa kwa mtu aliyekuwa akisafiri kutoka Uganda kwenda Rwanda kupitia Kenya.

Tahadhari 

Ili kuepuka maambukizi, watu wanashauriwa kuzingatia masharti ya afya wanapokuwa maeneo ya umma.

Vile vile, madaktari wanasisitiza umuhimu wa kunawa mikono kwa sabuni na maji mara kwa mara ili kulinda afya.

Watu wenye dalili za ugonjwa huu wanatakiwa kufuata miongozo ya afya.

Maelekezo haya yanashusisha kutokaribia wengine, kabla ya kufika katika kituo cha afya kilicho karibu kutibiwa.

Maambukizi haya huenea watu wanapokaribiana na waathiriwa wenye dalili za mafua na upele.

Kulingana na CDC, kwa sasa hakuna tiba mahususi iliyoidhinishwa ya maambukizi ya virusi hivi.

Kwa wagonjwa wenye kinga thabiti wasio na maradhi ya ngozi, uangalizi wa kawaida wa kudhibiti uchungu bila matibabu unaweza kuwasaidia kupona.

Chanjo ya Mpox inaweza kusaidia kuepuka maambukizi. Picha| Hisani

Kwa mujibu wa WHO, chanjo ya Mpox inaweza kusaidia kuepuka maambukizi.

Chanjo hutolewa ndani ya siku nne baada ya mtu kukaribiana na mwathiriwa (ama hadi siku 14 kama hakuna dalili).

Baadhi ya mataifa barani Afrika ambayo yameripoti kuwa na visa vya Mpox ni DRC, Burundi, Central African Republic, Nigeria, Afrika Kusini na Sierra Leone.

Kadhalika Visa vimeripotiwa katika mabara mengine duniani yakiwemo Ulaya, Asia, Amerika Kaskazini, Amerika Kusini, Asia, na Australia.