Habari za Kitaifa

Hatuwataki! Murkomen, Joho na Duale ndio wanaopingwa zaidi na Wakenya

Na SAMWEL OWINO August 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MIONGONI mwa mawaziri  walioteuliwa na Rais William Ruto Bw Kipchumba Murkomen, Bw Hassan Joho na Bw Aden Duale ndio wanaopingwa zaidi na Wakenya.

Bw Murkomen ameteuliwa kama wizara ya Masuala ya Vijana, uchumi wa ubunifu na michezo, Bw Joho (Madini na Uchumi wa Majini) huku Duale akiteuliwa Waziri wa Mazingira, mabadiliko ya hali ya hewa na misitu.

Kulingana na uchambuzi uliofanywa na Bunge na kuonekana na Taifa Leo, Bw kuna barua 92 za kupinga uteuzi wa Murkomen,  72 za kupinga Joho na 69 za kupinga Duale.

Wakenya waliwasilisha maombi 68 ya kupinga Waziri mteule wa Masuala ya Ndani Kithure Kindiki huku maombi 58 yakipinga  uteuzi wa David Chirchir ambaye amependekezwa Waziri wa Barabara

Waziri mteule wa Ulinzi Soipan Tuya alipingwa kupitia maombi 48 huku mwenzake wa Ardhi, Alice Wahome akipingwa  kupitia  malalamishi 40 yaliyowasilishwa dhidi ya uteuzi wake.

Wycliffe Oparanya alikuwa na maombi 33 yaliyowasilishwa dhidi ya uteuzi wake, John Mbadi, waziri mteule wa Fedha alikuwa na malalamishi 31, uteuzi wa Alfred Mutua (Leba na ulinzi wa kijamii) ulipingwa kupitia malalamishi 23, na Waziri mteule wa Elimu Julius Ogamba alipingwa kwa maombi 21 huku Salim Mvurya (biashara na uwekezaji) na Rebecca Miano (utalii na wanyamapori) wote wakipingwa kwa maombi 19 ya kupinga uteuzi wao.

Opiyo Wandayi ambaye ameteuliwa kuhudumu kama Waziri wa Nishati na Petroli alipokea maombi 11 ya kupinga uteuzi wake, Justin Muturi (utumishi wa umma) alipokea maombi 16, na mgombea wa Waziri wa Afya Debra Mulongo alikuwa na maombi sita ya kupinga uteuzi wake.

Margaret Nyambura Ndung’u ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia) na Andrew Mwhia Karanja (kilimo na mifugo) walikuwa na ombi moja tu la kupinga uteuzi wao.

Bunge lilipokea jumula ya malalamishi 1,368 kupinga uteuzi wa mawaziri hao.

Hata hivyo, jumla ya risala 157 zilizotumwa kwa njia ya barua pepe zilibainika kutozingatia kifungu cha 6 (9) cha sheria ya vibali vya bunge.

Kifungu cha 6 (9) cha Sheria ya Uteuzi wa Umma (Idhini ya Bunge), 2021 kinasema kwamba “mtu yeyote anaweza kabla ya kusikilizwa kwa idhini na kwa maelezo ya maandishi juu ya kiapo, kumpa karani ushahidi wa kupinga kufaa kwa mgombea kushika nafasi hiyo ambayo mgombea ameteuliwa.