• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Wizi mkubwa wa kahawa watia maseneta kiwewe

Wizi mkubwa wa kahawa watia maseneta kiwewe

Na GEORGE MUNENE

KAMATI ya Kilimo ya Seneti Jumanne ilielezea hofu yake kuhusiana na ongezeko la visa vya wizi wa kahawa nchini.

Kahawa ya thamani ya mamilioni ya fedha imeibwa kutoka kwa wakulima eneo la Mashariki katika siku za hivi majuzi.

Maseneta hao sasa wamemtaka Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai kuanzisha uchunguzi kuhusiana na visa hivyo mara moja.

Kamati hiyo ilisema wakulima wamepata hasara kubwa na wale waliohusika katika wizi wa zao hilo wanafaa kutambulishwa, kukamatwa na kushtakiwa.

‘Njia ya kipekee ya kukomesha wizi wa mazao ya wakulima yaliyohifadhiwa ni kukamata na kushtaki wahusika wote,” alisema mwenyekiti wa kamati hiyo Bw Njeru Ndwiga.

Akiongea wakati wa mkutano na wanahabari katika kiwanda cha kahawa cha Kiviuvi, Kaunti ya Embu, ambako wezi walivamia na kupora kahawa ya thamani ya zaidi ya Sh2.5 milioni, Bw Ndwiga alisema inahuzunisha kwamba wakulima wanaendelea kupoteza mazao yao kutokana na makundi ya wahalifu, bila yeyote kukamatwa.

“Wakulima wanataabika kwa sababu ya wizi wa kila mara wa kahawa. DCI inafaa kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha kuwa wote waliohusika wametambulishwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa kisheria,” alisema Bw Ndwiga.

Kamati hiyo ilipendekeza kuchunguzwa kwa wamiliki wa vinu vya kusaga kahawa ili kujua wanakotoa kahawa yao.

Alisema wamiliki hao wanafaa kulazimishwa kutoa stakabadhi na vyeti vinavyoonyesha walikonunua kahawa waliyohifadhi ndani ya mabohari.

“Tungependa kujua wanakotoa kahawa wanayosaga na kuuza,” alisema.

Wakati huo huo, kamati hiyo ilishutumu usimamizi wa shirikisho la vyama vya kahawa kwa kukataa kuchukua hatua za kutosha kulinda kahawa na kuongeza kuwa linafaa kuwajibika viwanda vinapovunjwa na kahawa kuibwa.

You can share this post!

Kizimbani kwa kuhadaa polisi alitolewa mimba alipotekwa...

Vipusa wazua kioja baa wakizozania bia ya polo

adminleo