Mipango yasukwa waathiriwa wa vita vya Shifta warudishwe nyumbani Lamu
MAJADILIANO kabambe yanaendelea kati ya serikali kuu, kaunti na wadau mbalimbali kwa lengo la kuwarejesha nyumbani waathiriwa wa vita vya Shifta vya miaka ya 1960.
Kati ya mwaka 1963 na 1967, vijiji zaidi ya 10 Lamu Mashariki vilisambaratika majangili wa Shifta walipovivamia, kuchoma nyumba, kuua na kujeruhi wakazi, na kuiba mali ikiwemo mifugo.
Miongoni mwa vijiji hivyo ni Ishakani, Kiunga, Mwambore, Rubu, Simambaye, Mvundeni, Ashuwei, Matironi, Mkokoni, Vumbe, Saadani, Kiangwe, Ndhununi na Bodhei.
Familia nyingi ambazo ni za jamii ya Wabajuni zilihama kutoka vijiji hivyo na hadi sasa hazijarudi tena makwao.
Baadhi ya familia hizo zilihamia kisiwa cha Manda, Mji wa Kale wa Lamu, Ngomeni, Malindi na Watamu, kaunti ya Kilifi, Mombasa, ilhali zingine zilielekea Tanzania na Uganda.
Katika mahojiano na Taifa Leo mnamo Ijumaa, Agosti 2, 2024 Naibu Kamishna wa Lamu Mashariki, Bw George Kubai, alisema serikali kuu imefanya kila jitihada kuhakikisha usalama unadumishwa katika vijiji vilivyoathiriwa na vita vya Shifta.
Operesheni za kudumisha usalama
Mbali na Shifta, magaidi wa Al-Shabaab pia wamekuwa kero kwa usalama vijijini humo.
Hata hivyo, Bw Kubai alisema kupitia operesheni inayoendelea msituni Boni visa vya Al-Shabaab kuonekana au kushambulia vijiji husika vimepungua pakubwa miaka ya hivi punde.
Operesheni hiyo inayoongozwa na Jeshi la Ulinzi Kenya (KDF) kwa ushirikiano na vitengo mbalimbali vya polisi nchini (NPS), ilizinduliwa rasmi Septemba 2015 dhamira kuu ikiwa kuangamiza kabisa wanamgambo hao wanaoaminika kujificha ndani ya msitu wa Boni.
“Ninafahamu fika kwamba kuna vijiji viliathiriwa pakubwa na vita vya Shifta. baadhi vimesalia na watu wachache huku vingine vikisambaratika kabisa. Mpango upo. Tunajadiliana na kaunti na wadau mbalimbali kuona jinsi tutasaidiana ili familia zilizohama zamani ziweze kurudishwa nyumbani,” akaeleza Bw Kubai.
Kamishna huyo alisema miongoni mwa mikakati inayoendelezwa kushawishi waliohama warudi kwa makazi yao, ni kuhakikisha usalama wa maeneo husika unadumishwa.
“Pia tunaboresha miundomsingi hasa barabara, elimu na afya. Tukifanya hivyo ninaamini walioathiriwa watakuwa na imani tena ya kurejea katika makazi yao ya zamani,” aliongeza.
Kwa upande wake, Msemaji wa Waathiriwa wa Vita vya Shifta katika Kaunti ya Lamu, Bw Mohamed Mbwana Shee, alisisitiza haja ya serikali na wahisani kuwajengea nyumba kwenye vijiji husika kabla ya kuwasaidia kiusafiri kurudi vijijini mwao.
Kulingana na Bw Mbwana, wengi wa waathiriwa wanaishi maisha ya umaskini na katu hawawezi kugharimia ujenzi wa nyumba na nauli ya kurudi vijijini mwao.
“Kwanza tufidiwe sisi waathiriwa wa Shifta. Baadaye tujengewe nyumba vijijini na kupokezwa misaada mingine ya kibinadamu kabla ya kuhamishiwa vijiji tulivyotoroka zamani,” akaeleza Bw Mbwana.