Kimataifa

Waziri Mkuu wa Bangladesh alemewa na maandamano ya Gen Z, atorokea India


DHAKA, Bangladesh 

WAZIRI Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina alijiuzulu Jumatatu, Agosti 5, 2024 na kutorokea India kufuatia maandamano yanayoendelea nchini humo.  

Duru zinaarifu zaidi ya 300 wameuawa katika ghasia mbaya zaidi kuwahi kutokea taifa hilo la Asia Kusini.

Mkuu wa jeshi Jenerali Waker-Us-Zaman alisema katika hotuba yake kwa njia ya televisheni kwamba Hasina 76, aliondoka nchini humo na kwamba serikali ya mpito itaundwa.

Vyombo vya habari vilisema kwamba alisafiri kwa helikopta ya kijeshi akiwa na dadake aliyekuwa akielekea India.

Kituo cha televisheni cha CNN News 18 kilisema alikuwa ametua Agartala, mji mkuu wa jimbo la Tripula Kaskazini Mashariki mwa India.

Reuters haikuweza kuthibitisha ripoti hizo mara moja.

Picha za televisheni zilionyesha maelfu ya watu wakimiminika katika barabara za mji mkuu Dhaka kwa shangwe na kupiga kelele.

Maelfu pia walivamia makazi rasmi ya Hasina ‘Ganabhaban’, wakipiga kelele na kuonyesha ishara za ushindi.

Picha za runinga zilionyesha umati wa watu kwenye vyumba vya makazi ya kiongozi huyo, na watu wengine walionekana wakibeba runinga, viti na meza kutoka kwa moja ya majengo yaliyolindwa zaidi katika nchi hiyo.