Maombolezo kijijini baada ya ngamia 100 kufa
Na GITONGA MARETE
ZAIDI ya ngamia 100 wamefariki katika mpaka wa Kenya na Ethiopia baada ya kunywa maji yenye sumu.
Dkt Shanda Guyo, afisa wa afya ya mifugo katika Kaunti ya Marsabit alisema ngamia hao ni wa kijijini El-Hadi, wadi ya Dukana katika eneobunge la North Horr.
“Tunashuku kuwa kisima hicho kilikuwa na maji hatari kwa afya ya mifugo kwa sababu kilikuwa kimetelekezwa kwa zaidi ya miezi miwili,” akasema.
Afisa huyo alisema kikosi kinachojumuisha madaktari wa mifugo na maafisa wa usalama kimetumwa katika kijiji hicho kilichoko takriban kilomita 300 kutoka mjini Marsabit, kwenda kufanya uchunguzi.
“Watachukua sampuli za maji ya kisima hicho ili kutuwezesha kufanya vipimo vya kina katika maabara,” akasema Bw Abduba.
Kifo cha ngamia hao kilisababisha hali ya huzuni kutanda kijijini hapo kwani jamii za wafugaji hutegemea pakubwa katika usafiri na shughuli nyinginezo za kila siku.
“Jamii za wafugaji zinathamini mno ngamia kiasi kwamba wanapofariki huomboleza. Baadhi ya ngamia waliokufa walikuwa na ndama na wafugaji wanahofia kwamba huenda wakafa pia,” akasema.
Ngamia mmoja huuzwa kwa wastani wa Sh120,000 na hiyo inamaanisha kuwa wanakijiji hao wamepoteza zaidi ya Sh12 milioni.
Wakati huo huo, viongozi kutoka Kaunti ya Marsabit wanataka serikali kuimarisha ulinzi huku wakisema kuwa wakazi wa eneo hilo wanaishi kwa hofu kutokana na tishio la magaidi.
Mkurugenzi Mkuu wa chama cha Frontier Alliance Party Barille Abduba aliitaka serikali kutuma maafisa wa kutosha wa usalama katika eneo hilo ili kudhibiti magaidi hao.
Bw Abduba alisema kuwa hali ya usalama katika eneo hilo inaendelea kuzorota kufuatia uwepo wa magenge ya wahalifu kutoka nchi jirani ya Ethiopia.
Kumekuwa na mashambulio kadhaa katika upande wa Marsabit baada ya jamii mbili kupigana.
“Tumekuwa tukiwapasha habari maaafisa wa kijasusi mara kwa mara lakini serikali bado haijachukua hatua yoyote,” akasema.