Kenya Power yaagizwa kufidia familia Sh2 milioni
KAMPUNI ya Umeme nchini (KPLC) imeagizwa kulipa fidia ya Sh2 milioni kwa familia moja jijini Mombasa ambayo nyumba yao iliharibiwa na moto katika ajali iliyotokana na utepetevu wa shirika hilo.
Familia ya Kassim Mbaya itapata fedha hizo kufuatia ajali iliyotokea miaka 12 iliyopita licha ya mahakama kugundua kuwa haikumiliki ardhi ambayo nyumba hiyo ilijengwa.
Mahakama ya Rufaa iliamuru kampuni hiyo ya umeme ilipe familia hiyo fedha hizo ikibaini kuwa dhana ya ‘nyumba bila ardhi’ inayotumika kwa kawaida katika eneo la Pwani ya Kenya haikuwa ngeni kwa mahakama kwani imetambulika na mahakama katika kesi za awali.
Hata hivyo, majaji wa mahakama ya rufaa Agnes Murgo, Dkt Kibaya Laibuta na George Odunga walipunguza fidia hiyo kutoka Sh3 milioni hadi Sh2 milioni, wakidai kuwa Mahakama Kuu iliyoshughulikia suala hilo awali ilizingatia baadhi ya mambo ambayo hayakupaswa kuzingatiwa wakati wa kutoa uamuzi wa madai ya uharibifu wa jumla.
Kwa mfano, majaji hao waliamua kwamba Jaji Patrick Otieno, alipokuwa akimtunuku Bw Kassim, alizingatia makadirio ya thamani ya bidhaa za nyumbani zilizoharibiwa katika moto huo.
“Kwa sababu hiyo, tumepunguza fidia hiyo kutoka kwa Sh3milioni hadi Sh2 milioni kwa usumbufu alioupata mlalamishi kutokana na moto ulioteketeza nyumba yao,” walisema majaji hao.
Babake Bw Kassim, Mzee Nzulwa, aliwasilisha kesi hii baada ya moto kuteketeza nyumba yake usiku wa Machi 6, 2012, kutokana na kuongezeka kwa umeme kutoka kwa laini za usambazaji umeme za KPLC iliyoko Barsheba, eneo la Kisauni.
Mzee Nzulwa aliilaumu kampuni hiyo kwa tukio hilo huku akisikitika kuwa kampuni hiyo ilizembea na kutojali katika uwekaji na utumiaji wa vifaa mbovu vya umeme na kushindwa kubadilisha, kukarabati au kurekebisha umeme huo.
“KPLC ilishindwa kutekeleza hatua zinazofaa za usalama ili kuzuia kuongezeka kwa umeme. Pia, ilishindwa kudhibiti moto huo kwa wakati ili kuzuia usiharibu nyumba yangu na vitu vya nyumbani,” alisema Nzulwa.
Mlalamishi alidai kuwa kutokana na kisa hicho cha moto, alibaki maskini bila makao na kuongeza kuwa KPLC ilikuwa na makosa yaliyosababisha hasara aliyopata.
Aliiomba kulipwa fidia ya Sh8 milioni kwa hasara aliyopata ikiwa ni pamoja na kupoteza vifaa vya kielektroniki, samani, nguo, vifaa vya nyumbani, vitu vya kibinafsi, na vifaa vya ujenzi, pamoja na gharama ya kujenga upya nyumba, mapato ya kukodisha; pesa taslimu; na vitu vingine mbalimbali.
Bw Nzulwa alifariki kabla ya kumalizika kwa kesi hii, hivyo mwanawe Kassim alisimamia kesi hiyo.
Kwa upande wake, KPLC ilikanusha kuwa uzembe wake ulichangia mkasa huo na kuongeza kuwa marehemu hakuwa mmiliki wa kiwanja hicho na nyumba inayodaiwa kuunganishwa na umeme.
“Iwapo marehemu alipata hasara , basi ilisababishwa na uzembe wake mwenyewe kwani alishindwa kumakinisha na kudumisha vizuia soketi za umeme vinavyofanya kazi vizuri katika majengo yake,” ilisema.
Aidha shirika hilo la umeme lilimtupia lawama marehemu kwa kuweka vifaa vingi vya umeme na kushindwa kuziba vizuri na kuzima kabisa vifaa vya umeme au kutunza mifumo ifaayo ya kuzuia ajali kama hiyo.
KPLC pia ilishutumu marehemu kwa kutumia nyaya zenye hitilafu kwenye majengo na kushindwa kufunga au kutunza vyema nyaya za umeme.