Kundi la wanazaraa Kibra linalokuza mimea bila kutumia udongo
KUNDI moja la wakulima kutoka mtaa wa mabanda wa Kibra, Nairobi umetambua mbinu maalum kuendeleza kilimo jijini bila kutumia udongo.
Muungano huo wa wakulima 60 unafanya kilimo cha kivungulio almaarufu greenhouse kwa kutumia malighafihai, kupitia mfumo wa hydroponics.
Hydroponics ni mfumo wa kisasa usiotumia udongo kuendeleza shughuli za kilimo, na unasifiwa kwa kudhibiti matumizi ya maji.
Vipandio vinavyotumika ni; coco pit, perlite, vermiculite, peat moss, clay pellets, grow stones, kati ya vingine.
Wanakuza pilipili hoho, nyanya na mseto wa mboga.
Wakulima hao walipata mafunzo kutoka kwa Shirika la Human Needs Project (HNP).
Msimamizi wao, kutoka HNP, Bi Stella Mwania, kwenye mahojiano na Akilimali Dijitali alisema waliingilia kilimo hicho wakati Kenya ilithibitisha kuwa mwenyeji wa Covid-19, mwaka 2020.
Hii ni baada ya wakazi wengi kuathirika kutokana na kazi zao kufungwa.
“Tuliwazia jinsi tungeweza kujiendeleza kimaisha, tukaishia kuchagua mfumo huu wa teknolojia ya kisasa,” alisema Bi Mwania.
Mfumo huo kando na kuwa rahisi, unatajwa kuzalisha chakula salama.
Mafunzo waliyopata yalifadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani la Muungano wa Umoja wa Kimataifa (FAO).
Kilimo cha hydroponics wanakifanyia katika vitongoji vya Olympic, Silverspring, Karanja na katika Shule ya Upili ya Kibra.
Mkulima Francis Otego kutoka kijiji cha Silverspring, alisema wana vivungulio 30, kila kivungulio kikimilikiwa na wakulima wawili.
Alisema hatua ya kwanza ili kumiliki ni kujisajiliwa.
“Nililipia Sh500 ili kupata mafunzo baada ya kupoteza kazi wa Covid,” alisimulia Otego.
Ni hatua iliyomuwezesha kukithi familia yake mahitaji muhimu ya kimsingi.
Yeye hulima pilipili hoho na nyanya.
Mkulima huyo anasema mimea hiyo hutumia aina mbili ya vipandio, na huwekwa mara mbili kwa wiki.
Katika kitongoji cha Olympic, pia tulikutana na Kevin Ooko aliyesifia mfumo wa hydroponics kwa sababu unapunguza matumizi ya pembejeo zenye kemikali.
Hata hivyo, ni muhimu shamba la mkulima kupimwa kiwango cha asidi na alikali – pH kabla kukumbatia teknolojia hiyo.
“Miezi mitatu baada ya upanzi, huanza kufanya mavuno,” akasema.
Mbali na soko la ndani kwa ndani nchini, wakulima hao huuza mazao yao ng’ambo.
Kilimo hicho kimerahihishia kazi wafanyabiashara wa mboga Kibra, kwani si lazima waende Marikiti, Nairobi kusaka bidhaa.