Bunge lataka Kenya Power igatuliwe kuwa kampuni nane za majimbo
KAMATI ya bunge inapendekeza Kampuni ya Kenya Power and Lighting Company (KPLC) igawanywe kuwa kampuni nane zihudumu kama mashirika yanayojisimamia katika iliyokuwa mikoa ya zamani kama njia ya kuongeza ufanisi kwa wateja.
Kamati ya Bunge ya Kitaifa kuhusu Kawi katika kikao na wasimamizi wa KPLC mnamo Jumanne ilisema njia ya pekee ya kuboresha ufanisi wa kampuni hiyo ni kuwa na mashirika mengi yanayofanya kazi kama kampuni huru.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Mwala Vincent Musyoka ilisema kusimamiwa kwa kampuni hiyo kutoka Nairobi kumefanya Wakenya wengi kulalamikia huduma duni.
Kuanzia kwa kukatika kwa umeme mara kwa mara, muda mrefu wa kusubiri kuunganishwa, kukosa kupandisha vyeo wafanyakazi na mengine mengi, kamati hiyo ilisema Kenya Power ina sifa mbaya miongoni mwa Wakenya ambayo lazima irekebishwe haraka.
“Je, unaweza kupendekeza kwamba serikali igawanye mamlaka ya KPLC kwa madhumuni ya ufanisi ili Wakenya wasilazimike kulalamika kila wakati?” akasaili Mbunge wa Nambale Geoffrey Mulanya.
Mbunge wa Gem Elisha Odhiambo alisema ili kuboresha utendakazi, afisi za sasa za kanda za KPLC katika maeneo manane i zinaweza kugeuzwa kuwa kampuni huru.
Bw Musyoka alisema kamati hiyo itaangazia sheria iliyopo na kuanza mchakato wa kugawanya kampuni hiyo akisema itahusisha washikadau wote ikiwa ni pamoja na kuwasilisha pendekezo hilo kwa umma kukusanya maoni.